KATIBU mkuu wa muungano wa wafanyikazi nchini COTU, Francis Atwoli amefananisha cheo chake kama cheo cha kuhani wa kanisa Katoliki.
Atwoli aliibua mfanano huo kupitia ukurasa wake wa X alipokuwa akijibu maswali kutoka kwa aliyekuwa gavana wa Makueni, profesa Kivutha Kibwana.

Akielezea safari yake katika kupigania haki za wafanyikazi hadi kufikia kuteuliwa kama katibu wao mkuu, Atwoli alisema kuwa kuwa katibu ni safari ya kukwea ngazi kama vile padre wa Katoliki anayekwea ngazi haki kufikia cheo cha Upapa.
“Kabla sijawa kiongozi wa chama cha wafanyakazi nilifanya kazi katika shirika la bango na mawasiliano la Kenya ambapo nilihudumu kwa miaka 19 na kisha miaka 7 kama Mkurugenzi wa Shirika katika COTU (K),” Atwoli alisema.
“Kuhudumu kama Katibu Mkuu wa COTU (K) ni wito. Ni sawa na Padre wa Kikatoliki kupanda vyeo na kuwa Papa katika Vatican. Masharti na mwenendo wetu wa utumishi umeegemezwa kwenye wito wa Mungu,” aliongeza.
Akionekana kudokeza kuwa bado hajachoka na uongozi wa muungano wa wafanyikazi, Atwoli alisema kwamba maadam wafanyikazi wana furaha chini ya uongozi wake, haoni haja ya kung’atuka.
“Na ili mradi bado nina uwezo na wenzangu bado wanafurahia utumishi wangu wataendelea kunichagua hadi wakati huo wafikirie vinginevyo,” alikariri msimamo.
Awali, alifichua kuwa chini ya uongozi wake, wafanyikazi wa kiume nchini sasa wanapata likizo za uzazi, kinyume na ilivyokuwa awali kabla ya ujio wa katiba ya 2010.
“Kwanza, nimepigania wafanyikazi [wa kiume] wa Kenya kupokea likizo ya uzazi kama sehemu ya kazi yangu kuleta seti tano (5) za sheria za Kazi. Unatambua kwamba sheria hizi na Katiba ya Kenya 2010, kama ilivyo katika Kifungu cha 41, zimempa mfanyakazi Mkenya mamlaka zaidi ya yote katika eneo hili,” alisema.
Mapema wiki jana, Francis Atwoli,75, aliripotiwa kukaribisha mtoto na mkewe Mary Kilobi, 40, baada ya kuwa katika ndoa kwa takribani miaka 7.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!