
MWANASIASA wa upinzani nchini Uganda, Bobi Wine amefichua jinsi mwenzake Kizza Besigye anavyoendelea katika gereza la Luzira.
Besigye amekuwa kizuizini kwa zaidi ya miezi minne sasa baada ya kukamatwa kinyemela Novemba mwaka jana jijini Nairobi na kusafirishwa hadi Uganda alikofunguliwa mashtaka ya uhaini katika mahakama ya kijeshi.
Bobi Wine alimtembelea Besigye katika gereza kumjulia hali na kufichulia umma kwamba afya yake imeimarika kwa kiasi kikubwa baada ya kusitisha mgomo wake wa kula zaidi ya mwezi mmoja uliopita.
“Leo alasiri katika Gereza la Juu la Luzira, tulimtazama mwenzetu mkuu, Dk. @kizzabesigye1. Tunafurahi sana kumpata akiwa na afya bora kuliko ilivyokuwa mara ya mwisho tulipojaribu kumuona,” Besigye alisema.
Wine alisema kwamba aliruhusiwa kuonana naye, na Besigye hakukaa kinyonge bali alimpa ujumbe wa kiharakati kufikishia wafuasi wake.
Kwa mujibu wa Bobi Wine, Besigye alimtaka kuwafikishia wafuasi wake ujumbe kwamba wasichoke katika harakati za kupambania haki sawa kwa kila mmoja kwani si yeye mfungwa pekee bali kila mtu katika taifa hilo la Uganda.
“Ujumbe wake kwetu sote ni kwamba lazima tubaki imara na tuwe na umoja zaidi katika kutafuta uhuru wetu. Anasisitiza jambo kwamba wafungwa kama yeye sio wafungwa pekee - sisi sote tuko chini ya utumwa kwa njia moja au nyingine,” Bobi Wine aliwasilisha ujumbe wa Besigye kwa wafuasi wake.
Besigye alisitisha mgomo wake dhidi ya kula mnamo Februari 23 baada ya kesi yake kuhamishiwa katika mahakama ya kiraia.
Alikuwa ameweka mgomo wa kula kwa siku kadhaa baada ya kuambiwa kwamba angepandishwa kizimbani katika mahakama ya kijeshi.
Hata hivyo, baada ya mawakili wake kufanya juhudi za kuona kesi yake ikihamishiwa katika mahakama ya kiraia kama alivyoomba, mwanasiasa huyo mkongwe wa upinzani alianza kula.
Alipofunguliwa mashtaka ya uhaini katika mahakama ya kiraia, ambapo hukumu yake ni kifo, alikanusha na kuzuiliwa zaidi hadi Machi 7 ambapo kesi hiyo ingeendelea.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!