Beatrice Elachi, Silvanus Osoro

MBUNGE wa Mugirango Kusini Silvanus Osoro ambaye pia ni kiranja wa walio wengi bungeni amefichua jinsi mbunge mwenza kutoka Dagoretti Kaskazini, Beatrice Elachi alichangia katika ukuaji wa maisha yake.

Akizungumza katika ibada ya wafu kwea ajili ya Elvis Murakana – mwanawe Elachi katika kanisa la Holy Trinity huko Kileleshwa, Osoro alisema kwamba wakati alifikia umri wa kuoa na alikuwa anatafuta mtu wa kuwakilisha marehemu mamake, Beatrice Elachi alijitokeza na kusimama naye katika nafasi hiyo.

Mbunge huyo wa Mugirango Kusini alieleza kwamba alipoteza wazazi wake wote akiwa na umri wa miaka 7 na kwa wakati Fulani maishani alilazimika kugeuka kuwa mtoto wa kuranda-randa mitaani.

“Nikiwa na umri mdogo wa miaka 7 nilipoteza wazazi wangu. Na nilijitafuta hadi kwa wakati Fulani ilinilazimu kuwa mtoto wa mitaani. Lakini kwa neema ya Mungu, leo hii tuko hapa.”

“Wakati nilihitaji mtu wa kuchukua nafasi ya mamangu wakati nilikuwa naoa, Beatrice Elachi alisimama na kuwa mamangu. Na hiyo ndio maana leo ninasimama upande wa familia. Amekuwa nguzo muhimu kwangu muda wote,” Osoro alisema.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Mbunge huyo alifafanua zaidi kiwango cha heshima yake kwa Elachi hata wakiwa bungeni licha ya kuwa kutoka pande tofauti za uongozi.

Osoro ni mbunge wa chama tawala cha UDA huku Elachi akiwa mbunge wa ODM.

Alisema kwamba huwa hazungumzi kwa ukali bungeni wakati anapomuona Elachi akiwa ameketi upande wa pili na hiyo ni kutokana na heshima aliyo nayo kwake kama ‘mama’.

“Wakati tunatofautiana, yeye [Elachi] huwa anashinda. Hata katika siasa kule bungeni ikiwa utapitia kwa Beatrice Elachi, huwa siwezi kuzungumza, badala yake nitatoka nje au nijifanye sijui ni nini kilikuwa kinazungumziwa. Na huwa sizungumzi kwa ukali wakati ninamuona bungeni,” Osoro alieleza.

Elvis Murakana Namenya alifariki kufuatia ajali ya barabarani mnamo Machi 25, 2025.

Alikuwa mwanafunzi wa Masomo ya Biashara katika Chuo Kikuu cha Africa Nazarene na alikuwa akisubiri kwa hamu kuhitimu mnamo Juni mwaka huu

Elvis alizaliwa Septemba 13, 1998, na atapumzishwa Machi 29, 2025.

Marehemu alikaa kwa wiki moja katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya AAR baada ya kuhusika katika ajali ya barabarani mapema wiki jana.

Inasemekana kuwa aliondoka nyumbani kuelekea Kasarani kwa shughuli zake mnamo Jumanne, Machi 18, ambapo ajali hiyo ilitokea.