
MBUNGE wa kuteuliwa, Sabina Chege amezua minong’ono kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuelezea alichokiona kaunti ya Bungoma mwezi Januari wakati wa mazishi ya mamake spika wa bunge Moses Wetang’ula.
Akizungumza Alhamisi asubuhi katika mahojiano kwenye kituo kimoja cha redio, Chege alisema kwamba alipigwa na butwaa kuona nyumba nyingi za matope katika kaunti hiyo ya Magharibi mwa Kenya.
Chege alisema kwamba hata alishangaa zaidi kuona kituo cha kibiashara kizima kikiwa ni nyumba za matope, zaidi ya hata idadi ya nyumba hizo katika uliokuwa mkoa wa Kati wote.
“Mapema mwaka huu wakati tulienda kwa mazishi ya mamake spika wa bunge Moses Wetang’ula, nilishangaa kugundua kwamba katika kaunti ya Bungoma, tuna nyumba nyingi za matope, kusema kweli kituo kizima cha kibiashara ambacho kimejaa nyumba za matope. Unajua Kati mwa Kenya hiki ni kitu ambacho hakijawahi sikika,” Chege alisema.
Mbunge huyo aliashiria kwamba eneo la Kati halina nyumba hizo nyingi za matope kwa kile alichoashiria kwamba wazazi wao walikuwa wachapa kazi ajabu.
“Nitakuambia uzoefu wangu wakati nilikuwa mdogo, tulikuwa na kahawa na majani chai, na mimi nililelewa na majani chai. Tungerauka asubuhi tunachuma majani chai na kisha tunaenda shuleni. Tukirudi jioni pia tungechuma majani chai ya kuweka usiku. Na tulifanya hii kazi kwa bidii sana,” aliongeza.
“Wazazi wetu sisi [kutoka Mlima Kenya] walifanya kazi kwa bidii sana, majani chai na kilimo kingine katika Mkoa wa kati wa Kenya vimeboresha sana maisha ya watu huko,” alisema.
Hata hivyo, Chege alibainisha kwamba hana maana kwamba Maeneo mengine ambayo aghalabu ni maskini, wazee wao hawakuwa wachapa kazi bali akasema inategemea na kilicho cha biashara ambacho kilikuwa kinakuzwa katika Maeneo yao.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!