Jackson Ole Sapit, askofu mkuu wa ACK

ASKOFU mkuu wa kanisa la Kiiangilikana la Kenya ACK, Jackson Ole Sapit amedai kwamba si ishara nzuri kwa wakenya kukuza hulka ya kusherehekea vifo vya watu mashuhuri kwenye mitandao ya kijamii.

Akizungumza kwenye runinga ya Citizen usiku wa Jumatano, Ole Sapit alisema kwamba katika siku za hivi karibuni, Wakenya wamekuwa na hulka hasi ya kusherehekea mambo mabaya kwenye mitandao ya kijamii.

Mkuu huyo wa Kidini alisema kwamba pengine ishara hii ni kuonyesha jinsi asilimia kubwa ya Wakenya wana hasira dhidi ya serikali ya William Ruto na kusema kwamba ni jambo linalostahili kusikilizwa na uongozi na kisha kutafutiwa suluhu.

Alikuwa akirejelea matukio ya hivi punde ambapo watu mitandaoni walionekana kusherehekea kifo cha aliyekuwa mwenyekiti wa tume huru ya mipaka na uchaguzi IEBC, Wafula Chebukati.

Pia wakenya walionyesha kusherehekea anguko la kinara wa ODM Raila Odinga ambaye alikuwa mgombea wa Kenya katika kinyang’anyiro cha uenyekiti wa AUC aliposhindwa na mgombea kutoka Djibout.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Kama hiyo haitoshi, siku moja iliyopita taarifa za kifo cha mwanawe mbunge wa Dagoretti Kaskazini Beatrice Elachi zilipokelewa kwa sherehe na baadhi ya watumizi wa mitandao ya kijamii.

“Ni hali ya kusikitisha sana kwa sisi [Wakenya] kujipata kwa hali kama hii, wakati maisha yamepotea haijalishi ni kwa njia gani, haifai kusherehekewa. Sidhani kama tunafaa kuwa na sababu yoyote ya kusherehekea kifo cha mtu yeyote kwa njia yoyote.”

“Na kusherehekea huku nafikiri kunatuma ujumbe Fulani, pengine kuna hasira iliyofunikwa ambayo inajengwa kwa njia kama hiyo – ambayo ninahisi haifai kuwa hivyo, lakini ni suala ambalo linafaa kushughuliwa kuhusu ni kwa nini Wakenya wana hasira kwa kitu chochote,” Ole Sapit alisema.

Kwa wiki ya pili sasa, Askofu huyo amekuwa akizuia wanasiasa dhidi ya kutoa hotuba katika mimbari ya kanisa za ACK akisisitiza kwamba hiyo ndio itakuwa kanuni katika kanisa zote.

Wikendi iliyopita, muungano wa makanisa humu nchini NCCK ulisisitiza kwamba wanasiasa hawafai kuruhusiwa kuwahutubia waumini kutoka kwenye mimbari ya kanisa.

NCCK pia ilikariri haja ya kutowekwa wazi kwa michango na sadaka ambazo wanasiasa wanatoa kanisani, wakiwakata kuheshimu utaratibu huo na kuhudhuria ibada kama waumini wengine.