
WAZIRI wa fedha John Mbadi amekariri kwamba janga kuu ambalo linazua kizingiti katika ukuaji wa taifa ni ufisadi.
Akizungumza wakati wa mazungumzo na wadau wakati wa kongamano lililoandaliwa na Taasisi ya Fedha ya Umma mnamo Machi 26, Mbadi alisema kuwa nchi inapoteza fedha nyingi kwa viongozi walafi na kutoa wito wa kuamsha fahamu za taifa katika kukomesha ufisadi na wizi wa umma.
Mbadi alisisitiza kwamba ili hayo yote kumalizwa, kila mtu aliyeko katika nafasi ya fursa ni sharti ajifunze kuwa na adabu ya kimwili, ufanisi na kukomesha wizi wa mali ya umma.
“Tumekuwa tukiita hili suala ufisadi. Huu ni wizi wa mali ya umma,” Waziri Mbadi alisema akirejelea mfano wa rais mstaafu Uhuru Kenyatta kwamba nchi ilikuwa inapoteza bilioni 2 kwa ufisadi kila siku.
Mbadi alisema kuwa ni kweli Kenya kuna kero la wizi wa mali ya umma, akitania kwamba Wakenya wanafanya vikao vya kupanga mikakati ya kuiba muda wote.
Waziri huyo alikariri kwamba Wakenya huwa hawana mapumziko katika kupanga mikakati ya kuiba mali ya umma, akisema kuwa huwa wanaiba si tu siku za wikendi lakini pia hata nyakati za usiku wakati wanastahili kuwa wamelala.
“Rais [mstaafu] Uhuru Kenyatta alisema kila siku Kenya tunapoteza bilioni 2 kwa ufisadi, niliona kwenye mitandao ya kijamii mtu akiuliza kama hiyo ina maana wakenya wanaiba hata wakati wa wikendi. Wakenya huwa hawalali, wanaiba hata nyakati za usiku niko na uhakika.”
“Mikutano mingi ambayo mnaona watu wanafanya kwenye mahoteli, ni kujadili mambo ya madili, hakuna kitu kingine. Wanapanga jinsi ya kuiba pesa,” waziri Mbadi alisema.
Waziri huyo pia alifichua kwamba wengi wa wale wanaoshiriki katika wizi wa pesa za umma ni watu wenye wako na uashawishi ndani ya serikali, akisema mtu wa kawaida akijaribu anakamatwa siku hiyo.
“Na unajua wanaoweza kuiba ni wale wa maana tu. Watu wa kawaida ukijaribu kuiba utashikwa siku hiyo hiyo," CS huyo aliongeza.
Mbadi alitoa wito kwa wenye hulka ya kuiba mali ya umma akisema kwamba ikiwa hawawezi kusitisha kabisa kuiba, basi wajifunze jinsi ya kupunguza wizi wao.
“Kama hatuwezi komesha wizi, basi tukubaliane kupunguza. Ni uamuzi wa fahamu ambao sijui kama tutakusanya kura ya maoni ama tutakwenda kanisani na kutubu tuseme ‘Mungu utatusamehe na tunaunguza wizi wetu kwa nusu. Kama nimekuwa nikiiba shilingi elfu moja, sasa ninaweka azimio kwamba nitakuwa ninabiba shilingi 500’. Hapo tutakuwa tumepunguza wizi kwa shilingi bilioni moja, na tutaokoa bilioni 365 kwa mwaka,” alisema.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!