
MSHAURI mkuu wa rais William Ruto kuhusu masuala ya uchumi Moses Kuria ametetea hatua ya Raila Odinga na wanachama wake wa ODM kutia saini ubia na serikali ya William Ruto.
Akizungumza katika hafla ya mazishi katika kaunti ya Tharaka Nithi, hafla ambayo ilihudhuriwa na viongozi kadhaa akiwemo Odinga, Kuria alisisitiza kwamba hatua ya Odinga kuungana na serikali haikuwa ya kukomboa eneo la Mlima Kenya bali kukomboa nchi ya Kenya.
Kuria alikariri kwamba wakati aliteuliwa kama waziri wa biashara, kitambo kabla ya ujio wa serikali jumuishi, aliona kulikuwa na nyufa kubwa katika serikali akisema kuwa aliona nchi ilikuwa inayumba.
“Unajua mengi yamesema kuhusu msimamo wa Raila katika siasa za hii nchi. Wakati niliteuliwa kama waziri, kitambo hata kabla ya ujio wa serikali jumuishi, nilikuwa na uwezo wa kuhiswi kuna jambo haliko sawa katika hii nchi. Na hatuwezi kuendelea na siasa uchochezi na migawanyiko,” Kuria alisema.
“Raila Odinga hakuja katika serikali jumuishi kuokoa watu kutoka Mlimani. Raila alikuja kukomboa nchi, na hiyo ndio tofauti kubwa. Wakati tulikuwa na shida na Gen Z na mnajua nini kilifanyika, Odinga alikuwa na chaguo mbili; alikuwa na kiberiti na petroli mkononi mwake, na alikuwa na maji katika mkono mwingine.”
“Alikuwa na nafasi ya kuchagua kutumia kiberiti na kuteketeza nchi, lakini alisema itanifaidi nini? Hivyo kwa mara nyingine, alirudi nyuma kuokoa hii nchi.”
Kuria alimhakikishia Odinga kwamba ataandamana naye katika kila swehemu ya nchi atakayozuru kuhakikisha taifa limeungana.
“Na Raila acha nikuhakikishie kwamba historia itakuhukumu kwa njia nzuri, na mimi mwenyewe nitaandamana na wewe popote uendapo mpaka tuhakikishe tumeunganisha hili taifa,” Kuria alisema.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!