
MAKACHERO wa upelelezi wa jinai, DCI wametoa taarifa kuhusiano na ripoti za kuwepo kwa raia wa kigeni wanaoshirikiana na wakenya kufungua maabara ya kutengeneza dawa za kulevya katika mji wa Namanga kaunti ya Kajiado.
Taarifa ya DCI ilijiri saa chache baada ya jarida moja la humu nchini kuchapisha simulizi kuhusu maabara hiyo ya kutengeneza dawa za kulevya iliyohusishwa na raia wa Mexico, Nigeria na Kenya.
Katika taarifa yao, DCI walikiri kwamba kulikuwepo na watu hao lakini msako wao mwezi Septemba mwaka jana ulifanikisha kukamatwa kwa baadhi yao ambao kesi inaendelea katika mahakama ndogo ya uwanja wa ndege, JKIA.
“Baada ya kuanzisha uchunguzi, mshukiwa wa kwanza (Mkenya) alikamatwa mnamo Septemba 16, 2024 katika nyumba yake Ruiru. Anaaminika kuongoza ujenzi wa maabara hiyo haramu kwa ushirikiano na mshukiwa wa pili (Mnigeria),” DCI walifichua.
Pia katika nyumba yake, walipata bidhaa kadhaa zikiwemo kemikali za kutengeneza dawa na idhibati za kununua shamba hilo la Namanga.
Uchunguzi wa kina ulibaini uhusiano kati ya Mkenya huyo na raia wawili wa Nigeria ambao pia walibainika kuwa na mawasiliano na raia wa Mexico ambaye aliwahi kuwa polisi nchini mwao.
“Uchunguzi pia ulituelekeza kwa mshukiwa wa 4, raia wa Mexico – afisa wa zamani wa kitengo cha upelelezi cha Mexico, alikamatwa katika uwanja wa JKIA akiwa mbioni kutorokea kwao.”
DCI ilibaini kwamba raia huyo wa Mexico ni miongoni mwa wengine wawili kutoka taifa hilo ambao waliletwa nchini Kenya na mshukiwa kutoka Nigeria.
Idara hiyo ilibaini kwamba upelelezi wao umebaini kwamba biashara ya kimataifa ya dawa za kulevya inayozungushwa kati ya mataifa ya Nigeria, India, Mexico, Gabon na Afrika Kusini.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!