Kawira Mwangaza

ALIYEKUWA gavana wa kaunti ya Meru, Askofu Kawira Mwangaza ametangaza kuwa ana jambo lake kuu kwa wafuasi wake usiku wa leo Machi 18.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Mwangaza aliwataka wafuasi wake kuwa ange kupokea tangazo lake ambalo aliweka wazi kwamba litakuwa ni tangazo lenye dhumni kuu la kisiasa.

“Leo usiku kupitia kurasa zangu za mitandao ya kijamii, nitakuwa natoa taarifa yenye madhumni ya kisiasa. Tafadhali jiunge na sisi kutoka starehe ya sebule yako kuanzia saa mbili usiku,” Mwangaza alichapisha.

Hii ni mara ya kwanza kwa gavana huyo wa zamani kuvunja kimya chake tangu kuapishwa kwa gavana mpya Jumatatu asubuhi.

Kuapishwa kwa gavana mpya – ambaye ni aliyekuwa naibu wa Mwangaza, Isaac Mutuma, kulimaliza kivangaito cha kisiasa cha zaidi ya miaka miwili ambacho kimekuwa kikishuhudiwa kati ya Kawira Mwangaza na bunge la kaunti ya Meru.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Masaibu ya Mwangaza yalianza miezi 5 tu baada ya kuapishwa kwake kama gavana baada ya kushinda kwa tikiti ya mgombea huru katika uchaguzi wa 2022.

Wawakilishi wadi walimbandua lakini seneti ikabatilisha uamuzi huo, lakini bunge la kaunti halikuridhika na lilirejesha hoja ya kutokuwa na Imani naye bungeni mwaka jana na hatimaye kumbandua tena.

Safari hii, Mwangaza alitupwa chini ya lori na seneti, japo uamuzi huo wa seneti ulipigwa breki na mahakama mnamo Agosti mwaka jana.

Uamuzi wa mahakama ulitolewa Ijumaa iliyopita ya Machi 14 na jaji Bahati Mwamuye ambaye alisema Mwangaza alipewa muda stahiki wa kujitetea kwenye seneti kinyume na pingamizi lake kwamba hakusikilizwa ipasavyo na maseneta.

Jaji hivyo alidumisha uamuzi wa seneti, kumaanisha kwamba Mwangaza alikuwa amebanduliwa ofisini rasmi na saa chache baadae, serikali ilichapisha notisi kwenye gazeti rasmi la serikali kuhusu kuapishwa kwa Isaac Mutuma.

Mutuma alikula kiapo Machi 17 katika hafla ambayo ilihudhuriwa na viongozi wa zamani na wa sasa katika nyadhifa mbalimbali kwenye kaunti hiyo.

Tetesi zinadai kwamba Mwangaza anatarajiwa kutangaza chama chake cha kisiasa, saa chache tu baada ya kujiondoa kwenye chama tawala cha UDA.