Morara Kebaso

MWANAHARAKATI na Mwanzilishi wa chama cha INECT, Morara Kebaso amewataka vijana wote wasio na ajira kukongamana pamoja naye katika bustani ya Uhuru mnamo Machi 24.

Katika video ambayo alichapisha kupitia ukurasa wake wa X, Kebaso alisema kwamba vijana wengi humu nchini hawana kazi, jambo ambalo limewafanya wengi hata kushindwa kuanzisha familia.

Alitoa wito kwa vijana wote wasio na ajira kuungana naye katika kongamano la kuonyesha serikali jinsi ajira ni adimu kwa vijana na kuanza kuishinikiza kuwapa kazi.

“Tumekuwa kwenye mstari wa mbele kusema kwamba vijana wa Kenya hawana kazi. Hawawezi kujilisha, hawawezi kuishi, wengine hata hawawezi kuoa,” Kebaso alisema.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

“Kama wewe ni kijana na huna kazi, tunaanza kongamano la vijana wasio na ajira ili kushinikiza vijana kupata kazi. Mnamo Machi 24, tutakuwa Uhuru Park kuanzisha makongamano hayo kote nchini,” aliongeza.

Mwanaharakati huyo ambaye alitangaza utayarifu wake kufanya kazi na mrengo wa upinzani akiungana na wenzake Martha Karua na wengine alisema kwamba utakuwa ni mwanzo wa mjadala mkuu wa kushinikiza serikali kutoa ajira kwa vijana.

‘Kama unaweza fika Jumatatu saa tatu asubuhi, acheni tuwanonyeshe ni vijana wangapi kwa kweli ambao hawana ajira na hawawezi pata njia ya kujilisha na hata kujikimu kimaisha,” Kebaso alisema.