
HUKU shule za upili zikitajwa kuwa na uhaba wa walimu waliohitimu kutoa mafunzo katika masomo ya sayansi na hisabati, watahiniwa wa KCSE ya mwaka 2024 waliofuzu kujiunga na vyuo vikuu wamehimizwa kusomea kozi hizo ili kuziba pengo lililopo.
Rai hii ilitolewa na naibu chansela wa chuo kikuu cha Zetech, Profesa Njenga Munene wakati wa hafla ya kuzindua kitivo cha kutoa mafunzo ya digrii katika masomo ya sayansi ili kuongeza idadi ya walimu katika taaluma hiyo.
"Tunatambua jukumu muhimu ambalo walimu wa sayansi wanatekeleza katika kukuza uchumi unaotegemea maarifa. Programu hii imeundwa sio tu kuwapa wanafunzi umilisi wa somo bali pia kuanzisha mbinu bunifu za ufundishaji ambazo zitabadilisha tajriba ya ujifunzaji shuleni,” alisema.
Kwa mujibu wa wasomi na washikadau katika sekta ya elimu, shule za upili nchini Kenya zimekuwa zikishuhudia uhaba wa takribani walimu laki moja wa kufunza masomo ya sayansi.
Upungufu huo umesababisha msongamano madarasani na ongezeko la utegemezi kwa waelimishaji wasiohitimu kikamilifu, hivyo kuathiri ubora wa ufundishaji katika masomo ya ufundi.
Baada ya kuona pengo hili pana katika ufunzaji wa walimu wa masomo haya, Zetech sasa imezindua kozi hiyo ambayo wanafunzi wanaolenga kuwa walimu wa sekondari wamehimizwa kukumbatia.
Profesa Munene alifafanua kwamba kitivo hicho kipya kitakuwa kinafundisha walimu wa sayansi zote yakiwemo masomo ya Hisabati, Fizikia, Kemia, Baiolojia, Jiografia, Elimu ya Kimwili na Afya, Sayansi ya Nyumbani, Kilimo, na Sayansi ya Kompyuta.
Pia itajumuisha mafunzo ya ujuzi wa maneno na vitendo, uchunguzi wa kisayansi, na kazi ya kimaabara ya vitendo, ikiwiana na matakwa ya mtaala mpya wa CBC.
Ingawa juhudi kama hizo zinatarajiwa kuchangia katika kushughulikia uhaba wa walimu, wataalam wa elimu wanahoji kuwa mabadiliko mapana ya kimfumo—ikiwa ni pamoja na kuboreshwa kwa uajiri wa walimu, malipo bora, na maendeleo ya miundombinu—yatakuwa muhimu kuunda suluhisho za muda mrefu kwa sekta ya elimu nchini Kenya.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!