Raila Odinga

RAILA Odinga amepinga vikali kauli za baadhi ya viongozi wanaoegemea mrengo wa aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua ambao wanamtaka kuungana nao ikiwa ana nia ya kuwania urais mwaka 2027.


Akizungumza katika hafla ya mazishi ya aliyekuwa rubani wa kijeshi James Gitahi Jumamosi, Odinga alisema kwamba yeye ameshinda urais katika chaguzi nyingi tu lakini ni vile hajawahi kutangazwa mshindi.


Alisisitiza kwamba nchini Kenya tangu ujio wa uhuru wa vyama vyama mwaka 1992, uchaguzi pekee wa urais ambao ulifanyika kwa haki na kweli ni ule wa 2002 wakati Mwai Kibaki alishinda kwa kura nyingi.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans


Alikuwa akirejelea kauli ya seneta wa Murang’a Joe Nyutu ambaye alimrai kuungana na Gachagua na Kalonzo kama kweli anataka kushinda urais 2027, akidai kwamba hiyo ndio njia pekee angeibuka mshindi.


“Naona huyo kijana kutoka Murang’a akisema eti ooh ukitaka kuwa rais kuwa na Gachagua na Kalonzo. Wewe hujui mahali tumetoka bwana, poa. Poa kabisa. Nchi hii inaweza kuchomeka ikiwa kama watu hawajitahadhari sana,” Odinga alimjibu Nyutu.


“Uchaguzi ambao umekuwa wa haki na kweli tangu tulete huu mfumo wa vyama vingi ni ule wa 2002. Hiyo peke yake. Hizi zingine zoote mnajua. Kwa hivyo usiniambie mimi eti sijui nataka nishinde. Mimi nimeshashinda mara nyingi, sijatangazwa tu! Si mliona juzi tulikuwa tunasema fungueni server, maanake tulikuwa tunajua ndani ya hiyo server kuna ukweli. Walifungua? Lakini muhimu ni kwamba Kenya ni kubwa na muhimu kuliko sisi wote,” aliongeza.


Akionekana kukashifu mihemko ya kisiasa inayoendelea humu nchini, Odinga alisema kwamba ipo haja ya Wakenya kujifunza kuishi kati ya sasa na wakati wa uchaguzi mkuu ujao, 2027.


Alisema kwamba ajenda 10 katika makubaliano ya ubia kati ya UDA na ODM yanalenga kuhakikisha kuna utulivu wa kisiasa humu nchini kwa kipindi kilichosalia kuelekea uchaguzi mkuu lakini pia kuhakikisha gharama ya maisha imeshuka, ushuru kupunguzwa na pia ufisadi kutokomezwa.


Kwa wiki mbili sasa tangu kutia Saini mkataba wa makubaliano ya kufanya kazi Pamoja na serikali, Odinga amekuwa akipata wakati mgumu kutetea ubia huo dhidi ya kauli kutoka kwa baadhi ya wafuasi wake kwamba aliwasaliti.