
KIONGOZI wa chama cha ODM, Raila Odinga ameendeleza msururu wa kutetea ukuruba wake mpya na rais William Ruto.
Akizungumza katika kaunti ya Machakos Jumamosi kwenye hafla ya mazishi ya aliyekuwa rubani wa kijeshi, Gitahi James, Odinga alisema kwamba ushirikiano wa ODM na UDA unanuia kuleta utulivu nchini, huku akiwasuta wale wanaoendeleza kauli za kutaka Ruto kung’atuka.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo mkongwe wa kisiasa, wale wanaotaka rais Ruto kung’atuka madarakani wanasema hivyo pasi na kutoa mwafaka wa baadae.
Odinga alisisitiza kwamba Wakenya wanafaa kujifunza kuishi kati ya sasa na mwaka 027 wakati wa uchaguzi, akisema kwamba lengo lake kuungana na rais lilikuwa kuhakikisha utulivu katika kipindi cha sasa na 2027.
Raila alisisitiza kwamba ajenda 10 ambazo walitia Saini wiki mbili zilizopita katika ubia mpya baina ya ODM na UDA zinalenga kutatua masuala tata yanayowakumba Wakenya kama vile ufisadi uliokithiri na gharama ya maisha ya juu bila kusahau ushuru uliopitiliza.
“Kenya ni kubwa kuliko sisi wote na demokrasia ni kitu muhimu sana ambacho ni mchakato wa mrai wa muda mrefu. Demokrasia sio kama kahawa ya mara moja ambayo utachemsha na kunywa kwa wakati huo.”
“Cha umuhimu ni kwamba Kenya inasalia Pamoja, hakuna haja ya kusema eti Raila asimame 2027, kama wakati huo Kenya itafika pale kama imechomeka. Wakenya wanafaa kujifunza kuishi kati ya sasa na 2027.”
“Unaona sasa Wakenya wengi wanaumia, gharama ya maisha iko juu, ushuru uko juu, mambo haya ya ufisadi yamepanda. Ndio sababu tukaweka ajenda 10 kwenye ule mkataba. Na zile ajenda 10 za mkataba sio usaliti. Sasa nyinyi mnataka tufanye namna gani? Mnasema Ruto aende! Ruto aende! Aende halafu nini ifanyike?” Odinga alihoji.
Odinga amekuwa akitetea ubia huo mpya dhidi ya kauli kwamba amewasaliti Wakenya, akisisitiza kwamba hajamsaliti yeyote kati ya wafuasi wake.
Wikendi iliyopita, Odinga alikuwa na wakati mgumu kuwashaishi wananchi katika uwanja wa Gusii kuhusu mkataba huo ambapo walionekana kuondoka kwa kughafilika.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!