William Ruto

RAIS William Ruto amewarai wananchi waendelee kumuongezea majina ya utani hata ikiwezekana yafike 10.

Akizungumza Ijumaa katika eneo la Eastlands wakati wa kukamilisha ziara yake ya wiki moja jijini Nairobi, Kiongozi wa taifa aliendelea kusisitiza kwamba yeye haoni ubaya na majina ya utani ambayo Wakenya wamekuwa wakimbandika.

Ruto aliyeonekana kujipigia debe kuchaguliwa kwa miaka mingine 5 katika uchaguzi wa 2027 ili kuongoza kwa miaka 10 kama rais, aliwaambia wananchi wamuongeze majina hadi 10 ili yatoshane na hiyo miaka.

Ruto aliendelea kunadi sera zake na miradi ambayo amekuwa akitekeleza tangu kuchaguliwa kama rais 2022, na kusema kwamba haoni ubaya wa kuongezewa majina kadri anavyoendelea kuchapa kazi.

“Majina ni mengi, lakini kazi mimi nitafanya. Naendelea kufanya na nyinyi mnaniongezea majina. Mimi naona mniongezee mpaka yafike 10 yatoshane na ile miaka. Ama mnasemaje?” rais alisema.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Ruto ambaye katika ziara yake ya Nairobi amekumbatia majina ya Zakayo na Kasongo alitangaza wazi kwamba amesikia kuna jina jipya amepewa la ‘El Chapo’ na kusema kwamba liko sawa.

“Sasa huyu Kasongo ni nani? Ati ni mimi? Halafu kuna lingine nimesikia linaitwa El Chapo. Hata hilo pia? Basi tuendelee na hayo majina tufanye kazi nzuri. Acha mimi nisomeshe Watoto, niwatengenezee Barabara, nipange ajira kwa hawa vijana na nyinyi kazi yenu iwe ni kunibandika majina, na tunaendelea, si namna hiyo?” Ruto aliongeza.

Alhamisi akiwa katika ziara ya maeneobunge ya Lang’ata na Kibera, Kiongozi huyo wa nchi alitaja baadhi ya majina ambayo amekuwa akibandikwa na Wakenya, si tu baada ya kuwa rais bali pia huko nyuma hata kabla ya kuwa rais.

“Sasa mimi nataka niwaulize, mlianza huko mkasema Hustler, halafu mkasema Survivor, kisha mkaenda jina lingine, Zakayo. Sasa nimesikia mmeongeza lingine, Kasongo. Sasa haya majina mtaongeza hadi yafike mangapi? Eeh? Bado mtaongeza lingine ama hayo yametosha? Haki nyinyi mko na maneno. Sasa nyinyi mnataka haya majina yangu yafike mangapi?”

“Mnataka yafike 10? Sasa nitaongeza William Kipchirchir Samoei Ruto Hustler Survivor Zakayo Kasongo...sijui nani. Anyway, ni sawa tu. Tuendelee. Ama mnasemaje bwana?” rais Ruto alitania.