
INSPEKTA Jeneraliw a polisi Douglas Kanja amevunja kimya chake baada ya vituo bandia vya polisi kugunduliwa katika kaunti za Uasin Gishu na Kakamega katika siku chache zilizopita.
Akizungumza na waandishi wa Habari Jumatano, Kanja alisisitiza kwamba ni makosa makubwa kwa raia kuchukua hatua ya kufungua kituo cha polisi bila kufuata taratibu husika.
“Mtu ambaye alifungua stesheni yake, kituo cha polisi, kwanza mimi niseme hayo ni makosa makubwa maana kuna taratibu zile zinafuatwa, wananchi wa hapa kwa mfano wakitaka kituo cha polisi, kuna utaratibu ambao utafuatwa,” Kanja alisema.
Mkuu huyo wa idara ya polisi alieleza kinagaubaga taratibu ambazo zinafaa kufuatwa ili kuanzisha kituo cha polisi katika eneo lolote ndani ya mipaka ya Kenya.
“Kuna kitu ambacho kinaitwa public participation, Pamoja na uongozi wa eneo Fulani ambayo wenyewe wanaona ni kweli tunahitaji kituo cha polisi ndio tuweze kuongeza usalama, halafu hilo pendekezo linapelekwa kwa kamati ya usalama kwenye sub-county, ambayo inaongozwa na DCC na wakuu wa polisi wa hilo eneo, na wale wengine ambao wako katika vitengo mbalimbali vya usalama.”
“Wanaikalia chini hiyo ripoti vile wananchi wanapendekeza kama kweli kituo cha polisi kinahitajika eneo hilo. Hilo wazo linaletwa mpaka linafika kwa inspekta jenerali wa polisi kule Nairobi na kweli sisi tukifuata ule utaratibu umewekwa na Katiba yetu, tunaona kweli inatakikana kuletwa kituo cha polisi hapa. Huo ndio utaratibu unaostahili kufuatwa na yule aliyefungua kituo chake cha polisi angefuata hivyo,” Kanja alitoa maelezo ya kina.
Taarifa hii inajiri siku chache tu baada ya mwanamume wa umri wa miaka 26 kufungua kituo binafsi cha polisi kijijini Cheboror kaunti ya Uasin Gishu.
Habari zinasema kuwa mtuhumiwa Collins Leitich, almaarufu Chepkulei, mkazi wa Kijiji cha Asis eneo la Ndugulu, alijitwika jukumu la kuanzisha kituo cha polisi cha doria kwenye jengo moja, na kufikia kupaka rangi jengo hilo kwa rangi rasmi za polisi, na hivyo kujenga hisia ya kituo halali cha ulinzi.
Kama hilo halitoshi, Jumatano kuliibuka ripoti zingine za kundi la vijana ambao walikuwa wanaendesha seli bandia ya polisi katika kaunti ya Kakamega.
Kundi hilo lilikuwa linawakamata na kuwazuilia wananchi katika vyumba vilivyotelekezwa na kuwatoza faini ya shilingi 300 ili kuwaachilia huru.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!