pingu

MWANAJESHI mmoja wa kike aliripotiwa kubakwa hospitalini alikokuwa amelazwa baada ya kupatwa na hitilafu ya kiafya akiwa mazoezini.

Tukio hili la kuajabisha na kusikitisha lilitokea nchini Zambia ambapo daktari alimbaka mwanajeshi huyo aliyepelekwa kwa huduma ya matibabu.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi, Maambo Hamaundu alithibitisha kutokea kwa tukio hilo jana na mhusika yuko chini ya ulinzi.

 

Wizara ya Ulinzi nchini humo ililaani yaliyojiri na kuwahakikishia umma kwamba hakuna mtu atakayelindwa katika uchunguzi huo.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

"Menejimenti ya Kituo cha Matibabu cha Maina Soko inashirikiana na uchunguzi wa Polisi ili haki itendeke," alisema mkuu wa wizara, Hamaundu.

Kulingana na vyanzo vya uhakika kutoka kwa Kituo cha Matibabu cha Maina Soko, mgonjwa huyo ni mwajiriwa wa Jeshi la Zambia ambaye aliugua wakati wa mafunzo na alipelekwa hospitali kwa matibabu.

Matukio ya madaktari kuwabaka wagonjwa hospitalini si mageni kwani humu nchini Kenya wiki kadhaa zilizopita, daktari mmoja katika kaunti ya Mombasa alituhumiwa kwa kumtendea unyama mgonjwa wa kike.

Daktari huyo alifikishwa mbele ya hakimu mkuu Alex Ithuku katika mahakama kuu ya Mombasa mapema Februari ambapo alishtakiwa kwa kosa moja la ubakaji.

Alishtakiwa kwa kumbaka mgonjwa saa kumi na moja asubuhi tarehe 31 Januari 2025 katika hospitali ya Pandya, ambaye alikuwa akitafuta huduma ya kusafisha damu katika kituo hicho.

Hata hivyo alikanusha shtaka hilo na kuachiliwa kwa dhamana na mdhamini wa kiasi sawa na hicho.

Shirika la kutetea haki za wanawake FIDA lililaani kisa hicho, likisema kuwa mwanamke huyo alibakwa hapo awali na mshukiwa huyo, na kutaka watu wengine zaidi wakamatwe ambao waliwatuhumu kwa kukwamisha mwenendo wa haki.

Shirika hilo lilitoa wito kwa DCI kufanya uchunguzi dhidi ya unyama huo na kutaka hatua kali za kisheria kuchukuliwa dhidi ya mtendaji kama njia moja ya kuzima kabisa visa vya dhuluma dhidi ya wanawake.