Mahakama

MAHAKAMA kuu ya Bungoma imetoa uamuzi wa kipekee na wa kushangaza kuhusu kesi ambapo wanaume wawili walikuwa wanazozania haki ya kulea watoto baada ya mama yao kufa.

Mahakama hiyo ilitoa uamuzi ulioshangaza baadhi ya watu kutoka jamii hiyo wakati iliamuru kwamba baba wa kambo ndiye mwenye haki stahiki ya kuishi na watoto na wala si baba mzazi.

Kwa mujibu wa kesi hiyo, watoto wawili waliokuwa wanazozaniwa na kina baba wawili walifiwa na mama yao mnamo 2021.

Baada ya kumzika mama, baba mzazi alijitokeza akiwa amejihami na vyeti vyao vya kuzaliwa, mpango wa bima ya elimu na uthibitisho wa kuweza kuwakimu kielimu.

Hata hivyo, watoto walidinda kumkubali na kusimama kidete na baba wa kambo, jambo lililopelekea kesi hiyo kuhamishiwa mahakamani.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

“Watoto hao walitoa ushahidi kuwa hawakujua mshtaki (baba mzazi) ni nani kwani hawakuwahi kumuona hapo awali na walipendelea kusalia chini ya malezi ya mshtakiwa (baba wa kambo),” ilisomeka hukumu hiyo kwa sehemu.

Mahakama iliarifiwa kwamba baba wa kambo alikuwa ameishi na watoto hao kwa takribani miaka 10 na japo ilithibitisha kwamba mshtaki ndiye alikuwa baba mzazi, iliamuru baba wa kambo kuendelea kuishi na kuwalea watoto hao.

Wakati wanaume wote wawili walipata hali ya malezi kwa watoto, mahakama ilimpa baba wa kambo haki kamili, huku baba mzazi akitakiwa kuwatembelea tu mara moja moja.

Majukumu yaligawanywa kwa baba mzazi kugharamia matibabu na ada za shule huku baba wa kambo akitakiwa kushughulikia huduma za kila siku kwa watoto.