Moses Kuria, mshauri wa masuala ya kiuchumi wa rais Ruto

MSHAURI Mkuu wa rais Ruto kuhusu masuala ya kiuchumi, Moses Kuria amekiri kwamba bima ya matibabu ya SHA haijakuwa kamilifu na ina mapungufu mengi tu.


Akizungumza Jumatano usiku katika runinga ya Citizen, Kuria alikiri kwamba mpango huo wa bima ya SHA una hitilafu nyingi akikiri pia kwamba huwa anamwambia rais kila wakati kuhusu vitu ambavyo vina mapungufu.


Alisema kwamba yeye, kama mtu Mkenya yeyote angependa kuona SHA ikiboreshwa na kutoa huduma za matibabu kwa kila mtu lakini kwa sasa hali si hivyo.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans


“Moses Kuria, wewe ni mtu mwerevu, na rais anakusikiliza, mbona humwaambii kwamba SHA haifanyi kazi?” Jeff Koinange alimuuliza.


“Nitamwambia asubuhi, na huwa namwambia kila wakati kuhusu vitu ambavyo havifanyi kazi. SHA sio timilifu, kuna baadhi ya vitu ambavyo mimi ningependa kuona vimeboreshwa,” Kuria alijibu.


Mbunge huyo wa zamani alifafanua vipengele viwili ambavyo angependa kuona vimeboreshwa katika mpango wa bima ya SHA.


“Ningependa kuona vipengele viwili vikiboreshwa, kwanza ni jinsi wakenya wanawasilisha malalamiko yao kuhusu jinsi SHA haifanyi kazi; iwe ni kuenda kwa hii hospitali na kurudishwa, au ni mfumo ulikuwa na hitilafu au ilichukua muda…”


“Sasa hivi ni neno letu [kama serikali] dhidi ya neno lao [wananchi]. Haifai kuwa hivyo,” Kuria aliongeza.


Mshauri huyo wa rais alisisitiza kwamba kwa sasa serikali imeboresha jinsi Wakenya wanaweza kuwasilisha malalamishi yao kupitia nambari ambayo imetengwa mahsusi kwa ajili ya hilo.