
SPIKA wa bunge la kitaifa, Moses Wetang’ula ameeleza sababu ya kumtwika mbunge wa Ikolomani Benard Shinali majukumu ya kuwafanyia kazi wananchi wa Eneobunge jirani la Malava kufuatia kifo cha mbunge wao, Malulu Injendi.
Akizungumza Jumatatu katika kijiji cha Lugusi Jimbo la Malava katika hafla ya kumuaga Mbunge Malulu Injendi, spika Wetang’ula alifafanua kwamba mbunge huyo alikuwa ameanzisha miradi mingi ambayo imebaki njia panda kufuatia kifo chake.
Ili kuhakikisha kwamba miradi ya Injendi inaendelea kwa faida ya watu wa Malava, spika Wetang’ula alimpa jukumu hilo mbunge wa Ikolomani, Benard Shinali na kumtaka kutekeleza majukumu yote katika ofisi ya mbunge wa Malava.
“Ili kufanikisha haya nilimwagiza Mbunge wa Ikolomani, Bernard Shinali kuchukua jukumu la afisi ya eneo bunge la Malava na kwa kushauriana nami kuwezesha programu zilizokuwa zikifanywa na mbunge huyo aliyetuacha ambazo zilijumuisha basari na miradi ya NG-CDF miongoni mwa miradi mingineyo.”
“Hii itasaidia kuhakikisha uendelevu wa huduma za wananchi wa Malava kabla ya kumchagua mbunge mpya kuchukua nafasi ya Mhe. Injendi,” Spika Wetang’ula alisema.
Injendi alifariki dunia takribani wiki mbili zilizopita baada ya kulazwa hospitalini kwa muda.
Kando na kutoa tamko hilo kwa Shinali, Wetang’ula pia alitoa wito kwa wanasiasa wenzake kukoma kuzua rabsha katika hafla za mazishi akisema hatua zao huleta uharibifu mkubwa wa vitu katika hafla hizo na kuweka mzigo kwa familia ya mwendazake.
“Nikiwataka viongozi kuheshimu wafiwa, niliwakumbusha kuwa nguvu za kisiasa hazitapatikana katika mazishi na kuwataka wenzangu kuzifariji familia za wafiwa badala ya kuwaongezea machungu kwa kusababisha fujo na uharibifu wa mali.”
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!