Martha Karua na Morara Kebaso

MWANAHARAKATI na mwanasiasa Morara Kebaso amemuomba kiongozi wa chama cha People’s Liberation Party, Martha Karua kumteua kama mkuu wa Tume ya Maadili na Kupambana na Rushwa EACC iwapo atakuwa rais mbele yake.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa chama hicho cha PLP jijini Nairobi, Kebaso ambaye ni Mwanzilishi wa chama cha INJECT alisema kwamba Kenya imejawa na ufisadi na ubadhirifu wa fedha za umma haswa chini ya utawala wa rais William Ruto.

Kebaso alisema kuwa pia yeye analenga kuwa rais wa Kenya lakini akamuomba Karua iwapo atatangulia kuwa rais mbele yake, basi asisite kumteua kama mkuu wa EACC.

Akionesha uchu wake wa kutumbua majipu katika idara mbalimbali za serikali, Kebaso alisema kwamba atanyoosha kila idara ya suala la ufisadi litakuwa la kusikika tu.

“Nimekuwa na bahati ya kutembea katika Maeneo mbalimbali humu nchini, jumla ya kaunti 32, na mheshimiwa [Martha Karua] mimi nataka kukuambia kwamba yale mambo yanaendelea hapa ni wizi mtupu bila kazi. Ni wizi kulia, kushoto na kati.”

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

“Hakuna kitu cha maana kinachoendelea katika taifa letu. Katika bajeti ya trilioni 3.9, asilimia 70 inaenda katika wizi na ubadhirifu wa fedha za umma. Na kama utaenda popote humu nchini, ni miradi iliyokwama baada yam ingine. Ufisadi umeua ugatuzi wetu, umemaliza fursa za vijana.”

“Mimi nina azma ya kuwa rais wa Kenya, lakini hilo ni kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Ni Mungu anapatiana uongozi, sio mimi wa kujipa mwenyewe. Kama utakuwa rais mbele yangu, kile kiti ambacho naomba unipe ni cha EACC. Mimi nataka kufanya kazi bila kulipwa, nipatie tu hiyo kazi na uzime simu uniache, nitawashughulikia [wezi],” Kebaso alisema.

Karua amezindua upya chama chake baada ya kukibadilisha jina kutoka NARC-K mwezi uliopita hadi PLP.

Katika hafla hiyo ya uzinduzi upya, kando na Kebaso, wanasiasa wakuu wengine ambao walikuwepo ni pamoja na aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua, kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka miongoni mwa wengine.