Ruto na Raila

RAIS William Ruto amedai kwamba hatua ya kiongozi wa ODM, Raila Odinga kuwania uenyekiti wa AUC, japo bila mafanikio, iliwaunganisha Wakenya wote pamoja.

Akizungumza katika ikulu ya Mombasa alikomkaribisha Odinga aliyerejea nchini baada ya kupoteza kinyang’anyiro cha AUC wiki iliyopita, Ruto alimshukuru kwa kuliwakilisha taifa katika ngazi za kimataifa.

“Ninajivunia kwamba Raila Odinga aliweka juhudi zote kuwa mwaniaji mwenye nguvu barani Afrika. Alifanya safari angani na barabarani akizuru mataifa mbalimbali kujipigia debe si tu kwa niaba yake bali pia kwa niaba ya Kenya,’ Ruto alisema.

“Uwaniaji wake uliwaleta pamoja Wakenya wote. Nafikiri uwaniaji wake ulivutia sapoti kutoka kwa mirengo yote ya kisiasa – watu kutoka serikali, upinzani na kila mtu. Tuliungana nyuma ya uwaniaji wa Raila Odinga kama mwenyekiti wa AUC,” rais aliongeza.

Mkuu wa taifa alichukua fursa hiyo kuwashukuru wote waliochangia kwa njia kubwa ama ndogo katika kutangaza azma ya Odinga katika kinyang’anyiro cha AUC.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Rais pia aliwashukuru wakuu wa mataifa 22 ambao walisimama imara ya mwaniaji wa Kenya katika raundi zote hadi alipojiondoa kunako raundi ya 6.

“Ningependa kuwashukuru ndugu zangu na marafiki zangu kote barani Afrika kwa ishara yao ya mshikamano na sapoti ambayo walionyesha kwa Kenya na kwa Raila Odinga ambaye alikuwa mgombea wetu.”

Raila Odinga alijiondoa katika raundi ya 6 baada ya kupata kura 22 dhidi ya kura 26 alizopata mshindani wake kutoka Djibout, Youssouf Mahmoud Ali.Youssouf hatimaye aliibuka mshindi katika raundi ya 7 ambapo alipata akidi hitajika ya kura 33 na kuchukua uongozi kutoka kwa Moussa Faki aliyekuwa anamaliza hatamu yake.