Bilionea Ned Nwoko na Muigizaji Regina Daniels

Muigizaji mashuhuri wa Nigeria, Regina Daniels, ameibua gumzo mitandaoni baada ya kufunga akaunti yake ya Instagram, hatua inayokuja huku kukiwa na uvumi wa mgogoro katika ndoa yake na bilionea Ned Nwoko.

Hatua hiyo imezua mjadala mkali miongoni mwa wanamitandao, mashabiki na wachambuzi wa masuala ya burudani, hasa baada ya ripoti kusambaa kwamba mume wake anahusishwa na ujauzito wa mwigizaji mwenzake, Chika Ike.

Kwa mujibu wa tetesi hizo, Nwoko anadaiwa kuwa baba wa mtoto ambaye Chika anatarajia na kwamba anapanga kumfanya mke wake mwingine.

Kwa miaka iliyopita, Regina na Nwoko wamekuwa wakionyesha mapenzi yao hadharani kupitia mitandao ya kijamii, hasa wakati wa sherehe muhimu kama Siku ya Wapendanao (Valentine’s Day).

Hata hivyo, mwaka huu hakukuwa na ishara yoyote ya kusherehekea siku hiyo, hali ambayo iliwafanya mashabiki wake kuanza kuhisi kuwa huenda kuna matatizo katika ndoa yao.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Pia, Regina hajatoa pongezi zozote kwa mumewe baada ya kuteuliwa kuwa mgombea wa nafasi ya seneta katika jimbo la Delta kupitia chama cha PDP (People’s Democratic Party). Kukosekana kwa uungwaji mkono wa wazi kumeongeza uvumi kuwa mambo huenda si shwari katika ndoa yao.

Hii si mara ya kwanza jina la Chika Ike linahusishwa na bilionea huyo. Mwaka 2020, kulikuwa na madai kuwa wawili hao walikuwa na uhusiano wa kimapenzi, lakini Chika alikanusha vikali uvumi huo, akisisitiza kuwa hana mpango wa kuwa mke wa Nwoko.

Hata hivyo, ujauzito wake wa sasa umefufua mjadala mpya kuhusu uhusiano wao, huku mashabiki wakitilia shaka hali ya ndoa ya Regina.

Kufungwa kwa akaunti ya Instagram ya Regina kumewafanya mashabiki wake wengi kuhoji sababu halisi ya kitendo hicho.

Wengine wanahisi kuwa huenda anapitia changamoto za ndoa na ameamua kujitenga na mitandao ya kijamii kwa muda. Baadhi wanadhani anaweza kuwa anapanga mabadiliko makubwa katika maisha yake na anahitaji utulivu wa akili.

Kwa sasa, hakuna taarifa rasmi kutoka kwa Regina Daniels au Ned Nwoko kuhusu hali yao ya ndoa. Hata hivyo, mashabiki wanaendelea kufuatilia kwa karibu, wakisubiri kuona ikiwa Regina atarudi mitandaoni na kufafanua hali halisi.

Tutaendelea kufuatilia habari hii kwa ukaribu na kukuletea taarifa zaidi kadri zinavyoibuka.