Ne-Yo na wake zake watatu

Mwanamuziki maarufu wa R&B, Ne-Yo, ameibua gumzo mitandaoni baada ya video yake akiwabusu wake zake watatu kusambaa.

Tukio hilo lilirekodiwa nyuma ya jukwaa kabla ya kupanda kuwatumbuiza mashabiki wake, na tangu hapo limezua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki wake na watumiaji wa mitandao ya kijamii.

Baadhi ya mashabiki wa Ne-Yo wamempongeza kwa kuwa wazi kuhusu maisha yake ya mahusiano ya wake wengi.

Wanadai kuwa kila mtu ana haki ya kuishi maisha anayoyataka ilimradi hakuna anayedhulumiwa. Wafuasi wake waliomsapoti wanasisitiza kuwa iwapo wake zake wanakubaliana na mpangilio huo wa maisha, basi hakuna tatizo.

Hata hivyo, wakosoaji wake wanasema kuwa kitendo hicho si cha heshima, hasa kwa mtu wa hadhi yake kwenye tasnia ya burudani.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Wengi wanahisi kuwa kwa kuwa Ne-Yo aliwahi kuwa kwenye ndoa ya kawaida na Crystal Renay kabla ya kutalikiana mwaka 2023, kubadili mtindo wake wa maisha ghafla na kuufanya hadharani kunaweza kuathiri taswira yake kwa mashabiki wa muda mrefu.

Katika mahojiano ya awali, Ne-Yo alieleza kuwa amechagua kuishi maisha yanayomfaa na kwamba hana nia ya kufuata kanuni za kawaida za mahusiano. “Monogamy [uhusiano wa mke mmoja] si kwa kila mtu,” alisema kwenye mahojiano na "Lemon Drop The Show" mnamo Novemba 2024.

Alisisitiza kuwa wake zake wote wanajua hali halisi na wamekubaliana na mpangilio huo.

Wake zake hao watatu, wanaofahamika kwa majina ya Bella, Arielle Hill na Phoenix Feather, nao wameonyesha kuwa wanamuunga mkono msanii huyo. Wanadaiwa kuwa wasanii wa mitandao kama OnlyFans na mara kwa mara huonekana naye katika hafla mbalimbali.

Tukio hili limeibua tena mjadala mpana kuhusu maadili, uhuru wa mahusiano, na jinsi jamii inavyoona uhusiano wa wake wengi.

×

Wakati baadhi wanahisi kuwa Ne-Yo anapotosha vijana na kuendeleza maadili potofu, wengine wanahisi kuwa ni haki ya kila mtu kuishi anavyotaka.

Kwa sasa, Ne-Yo anaendelea na ratiba yake ya muziki huku tukio hili likiendelea kuchochea mijadala mitandaoni. Swali linalosalia ni je, jamii inapaswa kukubali mahusiano yasiyo ya kawaida kama haya, au bado tunapaswa kushikilia mila na desturi zilizokuwepo?