ALIYEKUWA naibu rais Rigathi Gachagua amezungumzia dhana midomoni mwa wakenya wengi kwamba hawezi kuwania wadhifa wowote wa kisiasa nchini Kenya haswa baada ya kubanduliwa mamlakani Oktoba mwaka jana.
Akizungumza asubuhi ya Jumanne Februari 4 na stesheni za jamii ya Abaluhya, Gachagua alisema kwamba hata kabla ya mchakato wa kubanduliwa kwake, baadhi walimsihi kujiuzulu ili kunusuru mustakabali wake wa kisiasa.
Alisema kwamba alikataa kujiuzulu kwa sababu hata hajipendi kama ambavyo baadhi ya watu wanafikiria, akisema kwamba hata harakati zake sasa hivi kupinga serikali si kwamba analenga kuwa chochote nchini.
Kiongozi huyo alifichua kwamba masaibu yake na rais Ruto yalianza pale alipoamua kusimama na kumuambia ukweli wakati watu wengine karibu naye walikuwa wanashindwa kumwambia.
“Yeye ndiye rais wa Kenya na mimi nilikuwa msaidizi wake. Lakini hilo halikunitoa katika haki ya kuongea kwa sababu pia mimi ni Mkenya na katiba inakubalia kila mtu kusema ukweli. Shida ilikuwa kila mtu anaambia rais ‘ndio’ ile inaitwa Praise & Worship Choir, mimi nilikataa kuingia katika hiyo kwaya nikiwa namwambia ukweli vile raia wanasema,” Gachagua alisema.
“Mambo ya kwamba eti nikifukuzwa sitasimama kiti hiyo haina maana kwangu. Mimi najua watu wanafikiria kwamba mimi ni mtu najipenda sana, sio lazima niwe chochote katika Jamhuri ya Kenya,” aliongeza.
Gachagua aliibua kauli yenye ukakasi kwamba rais Ruto hata alifikia hatua ya kumuahidi shilingi bilioni 2 ili kujiuzulu badala ya kungoja kung’atuliwa mamlakani, lakini akakataa.
“Na mimi hata ningesikiliza vile rais alikuwa ameniambia nijiuzulu kwa sababu alikuwa ameniambia ‘wewe jiuzulu nikupatie bilioni 2 uende nyumbani uende upumzike ufanye mambo yako, ukuwe na walinzi, ukuwe na mshahara na unaweza simama siku nyingine’…sasa nikajiuliza, yule anayekupangia mabaya anaweza kukupa suluhisho jinsi utaishi?” alisema.
Gachagua alisema si rais tu alimrai kujiuzulu ili kuweka hai mustakabali wake wa kisiasa, akisema kwamba hata baadhi ya wabunge wale wanaomuunga mkono walimtaka kujiuzulu pia badala ya kungoja kubanduliwa.
“Waliniambia nijiuzulu nikasema hiyo ni kujipenda, sio lazima nisimame, sio lazima niongoze, mimi lazima nitetee wakenya na ukweli ujulikane,’ aliongeza.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!