TAJIRI nambari moja duniani, Elon Musk amekuwa mtu maarufu kutoka nje ya Afrika wa kwanza kutia neno kauli ya rais mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta kuzitaka nchi za Afrika kuacha manung’uniko baada ya Marekani kutangaza mipango ya kusitisha misaada.


Kupitia ukurasa wa X, jukwaa analolimiliki, Musk alinukuu video ya Kenyatta akirai mataifa ya Afrika kuacha kulia baada ya Trump kutangaza misaada nje ya Marekani kusitishwa.


Kwa mujibu wa Musk, kauli ya Uhuru Kenyatta ni nzuri si tu kwake bali pia kwa mataifa mengi ya Afrika ambayo yamekuwa yakitegemea misaada ya mashirika na serikali ya Marekani kama USAID.


Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

“Ni vizuri kwake,” Elon Musk alinukuu video hiyo.


Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Januari, Uhuru Kenyatta akizungumza baada ya rais Trump kutangaza kusitishwa kwa misaada ya kimatibabu kuja barani Afrika, aliwataka Waafrika kuacha kulalamika kwa sababu Trump si rais wao.


Kwa mujibu wa Kenyatta, Waafrika hawafai kunung’unika Amerika kukata misaada kwao kwani hawalipi kodi nchini Marekani na wala Trump si rais wao.


"Niliona watu wengine siku nyingine wakilia kwamba Trump ameondoa ufadhili. Si serikali yako, wala nchi yako—mbona unalia?” Uhuru alipiga kwenye mshono.


“Hana sababu ya kukupa chochote; haulipi ushuru huko Amerika. Huu ni wito wa kukuamsha kujua mtakachofanya ili kujikimu,” Kenyatta alisema.


Kenyatta zaidi alisihi mataifa ya Kiafrika kuanzisha mifumo ya kifedha inayojitegemea kushughulikia majanga kama vile magonjwa ya milipuko, badala ya kuegemea wafadhili wa Magharibi.


Alisisitiza jinsi utegemezi wa kupita kiasi wa usaidizi wa kigeni umedumaza maendeleo ya kiuchumi ya Afrika na utulivu wa muda mrefu.


"Tutake au tusipende, ufadhili wa haya (magonjwa) lazima utoke kwetu kwa sababu inabidi tuanze kutanguliza tena kile ambacho ni muhimu kwetu kama Waafrika," Kenyatta alisisitiza.


Hata hivyo, siku moja baada ya Trump kutangaza kusitishwa kwa misaada, alibatilisha amri hiyo na kuruhusu misaada hiyo haswa ya kimatibabu kusambazwa kwa hadi mataifa 55 kote duniani yenye uhitaji mkubwa.