SENETA wa kaunti ya Nandi ambaye pia ni kada wa kudumu wa chama cha UDA, Samson Cherargei amezua mjadala pevu kwenye mtandao wa X baada ya kutoa kauli kwamba chama hicho kitasalia madarakati kwa hadi karne moja.


Cherargei, mtetezi mkali wa sera za serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na rais William Ruto alidai kwamba chama cha UDA kiko imara mithili ya Simba.


Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Alifuatisha kauli hiyo na picha yake akiwa amevalia sare rasmi za chama hicho – manjano, na kusema kwamba kauli zinazoenezwa kwamba UDA kimepoteza umaarufu na uungwaji mkono nchini katika miaka ya hivi karibuni ni kauli zisizo na ukweli wala mashiko.


 Alisema UDA ni chama ambacho kimejikita vyema katika siasa za Kenya na hicho ndicho kigezo ambacho kitakifanya kusalia mamlakani kwa miaka 100 ijayo.


“Chama tawala kikoi mara kama simba na wheelbarrow, na kitasalia kwenye uongozi kwa miaka 100,” Cherargei alisema.


Kauli hii inaonekana kuwa jibu kwa baadhi ya wanasiasa ambao katika siku za hivi karibuni wameonekana kujumuika Pamoja kwa lengo la kuanzisha miungano mipya inayolenga kumng’oa Rais Ruto mamlakani kupitia kura za mwaka 2027.


Wiki iliyopita, aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua alikutana na kiongozi wa chama cha NARC-Kenya Martha Karua katika kaunti ya Kirinyaga ambapo walitangaza kuja Pamoja kwa nia moja kisiasa.


Siku mbili zilizopita, Gachagua pia alikuwa miongoni mwa wanasiasa waliojumuika katika mtaa wa Karen katika uzinduzi wa ofisi kuu za chama cha DAP-K kinachoongozwa na aliyekuwa Waziri Eugene Wamalwa.


Hata hivyo, miungano hii haionekani kumyumisha kivyovyote vile rais Ruto ambaye amekariri kauli kwamba wanaotaka kushindana naye katika uchaguzi wa 2027 wana kazi nguvu sana.


Ruto alikariri kauli hiyo wiki mbili zilizopita wakati wa ziara yake ya maendeleo ya wiki moja katika ukanda mpana wa Magharibi mwa Kenya ambapo alisema washindani wake watakuwa na mchongoma wa kuukwea kushindana naye.