MBUNGE wa Embakasi Mashariki Babu Owino ameonyesha sikitiko lake kwa wakaazi wa Nairobi na haswa watumizi wa barabara nyakati hizi za mvua nyingi.


Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Babu Owino alichapisha picha ya mwendesha bodaboda mmoja aliyepigwa picha akijaribu kuiokoa pikipiki yake kutoka dimbwi la maji barabarani.


Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Owino alisema kwamba ni sikitiko kubwa kwa mwendesha bodaboda huyo kwani sasa huenda pikipiki yake imeharibika injini kutokana na kuzama kwenye maji barabarani.


Mbunge huyo anayedaiwa kuwa mbioni kujitosa katika kinyang’anyiro cha ugavana Nairobi alionekana kuulaumu uongozi wa jiji akisema kwamba gavana Sakaja ameshindwa kazi.


Owino alisema kwamba Sakaja ameshindwa kutatua suala la mabomba ya kupitisha maji chafu na kusababisha mafuriko kushuhudiwa kwenye barabara nyingi za Nairobi pindi mvua zinaponyesha.


“Moyo wangu unauma ninapomuona huyu mwendesha Bodaboda anayetegemea mashine hii kujipatia riziki; kulipia karo ya shule kwa watoto wake, kununua chakula, kulipa karo ya kila mwezi na kulipia gharama nyinginezo.”


“Mtu huyu anapata takriban 200/- tu kwa siku baada ya kununua mafuta lakini pikipiki yake haitafanya kazi tena kwa sababu injini imezama ndani ya maji kutokana na mfumo mbovu wa mifereji ya maji jijini Nairobi ambayo inaletwa na Uongozi duni kutoka kwa Gavana asiye na uwezo.”


“Wengi wa waendesha Bodaboda huchukua pikipiki hizi kwa mkopo na lazima walipe bila kujali hatari yoyote ya kikazi inayowapata. Tuna jumla ya bajeti ya shilingi Bilioni 42 lakini Gavana hafanyi lolote, ni mzuri tu kwa visingizio. Wanairobi wasimchague tena asiye mwanataaluma katika Nafasi hii. #Nairobi inazama,” Owino alisema.


Katika kipindi cha wiki moja, Nairobi sawa tu na maeneo mengine nchini yamekuwa yakishuhudia mvua nyingi ambazo idara ya utabiri wa hali ya hewa imesema kwamba mvua hizo zitakata kuanzia wikendi hii.