Mwanasiasa na mwanaharakati marufu David Morara Kebaso mnamo Jumatano aliadhimisha miezi mitatu ya kutoomba pesa kutoka kwa Wakenya.

Katika taarifa kwenye mtandao wa X, kijana huyo mwenye umri wa miaka 29 aliomba umma kuungana naye katika kusherehekea hatua hiyo kubwa.

"Nisaidieni kusherehekea miezi 3 bila kuomba michango yoyote kutoka kwa umma," Morara aliandika kwenye akaunti yake ya X.

"Ninatumai kwamba siku moja mtabadilisha mtazamo wenu kuhusu ufadhili wa umma na jukumu linalochukua katika kukomesha uchaguzi wa wafisadi," aliongeza.

Mara ya mwisho ambapo Morara alionekana kuomba fedha hadharani ilikuwa mwezi Oktoba wakati alipoomba kusaidiwa kuimarisha usalama wake. Hii ilikuwa baada ya shambulio kupangwa dhidi yake katika Bomas of Kenya.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Wakati akitoa ombi hilo, mwanaharakati huyo aliweka wazi kuwa hangefichua hesabu za fedha hizo kwa kuwa jambo hilo lilihusisha usalama wake na ni watu wenye mapenzi mema tu wanaomwamini wanapaswa kuchangia.

"Ninaomba Wakenya wa nia njema waniunge mkono katika kuimarisha miundombinu yangu ya usalama na wafanyikazi," aliandika Morara.

Mnamo mwezi Novemba, kiongozi huyo wa chama cha INJECT alitoa mchanganuo wa jinsi alivyotumia pesa zilizokusanywa na Wakenya kufuatia maombi yake ya mara kwa mara.

Katika taarifa yake, alifichua kuwa kati ya michango hiyo, ameajiri watumishi 23 wa kudumu na wanaolipwa mishahara, wengi ambao alisema ni watafiti na makarani wa data.

Mwanaharakati huyo alibainisha kuwa amefanya mikutano 27 ya elimu ya uraia kote nchini na kwamba fedha zilizokusanywa na Wakenya zimesaidia katika kuweka mafuta kwa magari yaliyotumika katika zoezi hilo.

"Tumefanya mikutano 27 ya elimu ya uraia katika kaunti mbalimbali. Kati ya michango yenu mikubwa tumeajiri wafanyikazi 23 wa kudumu na wanaolipwa mishahara, wengi wao wakiwa wa usalama, watafiti na makarani wa data.Michango yenu imehudumia magari mawili kama ifuatavyo: KDK kwa takriban kilomita 29,000 na KCJ kwa takriban kilomita 20,000," Morara alisema.

Morara alisema kuwa amezuru kaunti 29 na kukagua miradi 89 ya serikali, ambayo alidai ilitengewa takriban Ksh137 bilioni.

"Tunasikitika kuripoti kwamba uchambuzi wetu kufikia sasa unaonyesha kuwa Wakenya walipoteza takriban bilioni 96 katika miradi ambayo tumetembelea. Hiyo ni takriban asilimia 70 ya bajeti iliyoibiwa," Morara alidai.

Mwanaharakati huyo aliendelea kutafuta sapoti kutoka kwa Wakenya katika mazoezi yake ya elimu ya uraia na kudai kuwa chama chake cha siasa cha INJECT ni chumba cha kutotolesha viongozi wajao.