TAKRIBANI miezi 11 tu baada ya kuondoka ofisini, rais wa zamani wa Nigeria, Muhammadu Buhari amezua mjadala baada ya kukiri kwamba yeye si tajiri.


Rais huyo mstaafu aliwashangaza wengi alipoungama kwamba baada ya kumaliza miaka 8 ya urais, sasa anaishi maisha ya kutegemea kodi za nyumba kutoka kwa wapangaji wake.


Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Muhammadu Buhari alisema kuwa familia yake sasa inategemea mapato kutokana na kupangisha moja ya nyumba zake mbili katika Jimbo la Kaduna, akisisitiza kuwa "sikujitajirisha kwa rushwa kama rais."


Kwa mujibu wa Sahara Reporters, Buhari alitoa madai haya alipokuwa akihutubia mkutano wa wanachama wa All Progressive Congress (APC) katika Jimbo la Katsina siku ya Jumapili, kabla ya uchaguzi wa baraza la mtaa wa jimbo hilo uliopangwa kufanyika Februari 15.


Alisisitiza kuwa aliondoka madarakani bila utajiri wowote alioupata kinyume cha sheria, akibainisha kuwa Nigeria ni nchi ngumu kutawala kutokana na ugumu wake.


Akizungumza kwa lugha ya Kihausa, rais huyo wa zamani alisema kuwa Wanigeria wengi hawakufahamu changamoto za kiutawala zinazohusika katika kutawala nchi, lakini wanalaumu tu viongozi.


"Nigeria ni nchi ngumu kutawala, lakini Wanigeria wengi hawajui. Mpaka ujipate katika nafasi ya utawala wa nchi, ikiwa sivyo, huwezi kuelewa magumu.”


“Naonekana bora na mwenye afya tele sasa kuliko nilipokuwa rais wa nchi. Yeyote anayeniona sasa anakubali kuwa ninaonekana bora kuliko hapo awali," Buhari alisema.


Aliongeza, “Baada ya miaka minane nikiwa rais wa serikali, nina nyumba tatu tu; moja huko Daura na mbili Kaduna. Nimetoa moja kwa ajili ya kukodisha ambapo napata pesa za kulisha familia.”


Mnamo 2015, kama rais wa Nigeria, Buhari alitangaza mali yake, akisema ana nyumba tano na nyumba mbili za udongo.