SERIKALI ya Kenya kupitia katibu katika wizara ya masuala ya kigeni, Korir Sing’oei imeonyesha kusikitishwa kwake na mashambulizi ya ubalozi wa Kenya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC.
Kwa mujibu wa Sing’oei, waandamanaji walivamia na kuharibu vitu katika makao makuu ya ubalozi wa Kenya jijini Kinshasa.
Katika taarifa ya Jumanne, Januari 28, Katibu Mkuu wa Masuala ya Kigeni Korir Sing'Oei alilaani mashambulizi hayo na kuyataja kama ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa.
Alibainisha kuwa waandamanaji hao, waliokasirishwa na mzozo unaoendelea mashariki mwa DRC, pia walilenga balozi za Uganda na Afrika Kusini.
"Tunasikitishwa sana na mzingiro na mashambulizi yanayoendelea kwenye Majengo ya Ubalozi na wafanyakazi huko Kinshasa, DRC, ikiwa ni pamoja na Balozi za Kenya, Uganda na Afrika Kusini, kwa waandamanaji wanaoonyesha kutoridhika kwao na mzozo wa Mashariki mwa nchi hiyo. Maendeleo haya ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na tunalaani kwa maneno makali iwezekanavyo," alisema.
Sing'Oei alizitaka mamlaka nchini DRC kuchukua hatua za haraka na zinazofaa kurejesha utulivu na kuhakikisha usalama wa balozi za kidiplomasia.
"Tunatoa wito kwa mamlaka nchini DRC kuchukua hatua zinazofaa. Kenya inasimama na DRC wakati huu wa changamoto na itatumia njia zote za kidiplomasia zilizopo kufanya kazi na eneo lote katika kutafuta amani," aliongeza.
Sing'Oei pia alitoa onyo kwa raia wa Kenya na wafanyabiashara nchini DRC, na kuwashauri kuwa waangalifu wakati wa machafuko.
"Tunawasihi raia wa Kenya na wafanyabiashara kuchukua tahadhari katika kipindi hiki," akamalizia.
Mnamo Jumatatu, Januari 27, maandamano yalizuka mjini Kinshasa huku raia wakitoa hasira zao kutokana na mzozo unaozidi kuongezeka katika maeneo ya mashariki.
Machafuko ya mjini Kinshasa yalichochewa na mashambulizi ya hivi karibuni ya waasi wa M23 katika mji wa mashariki wa Goma.
Waasi hao wamezidisha shughuli zao, huku kukiwa na ripoti za milio ya risasi na milipuko na kuwalazimu maelfu kukimbia.
Rais William Ruto ni miongoni mwa viongozi wa Afrika Mashariki ambao wametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa uhasama na juhudi mpya za kuleta amani Mashariki mwa DRC.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!