KIONGOZI wa wengi katika bunge la kitaifa ambaye pia ni mbunge wa Kikuyu, Kimani Ichung’wah ameteuliwa kuwa ajenti mkuu wa Raila Odinga kwenye uchaguzi wa AUC mwezi ujao.
Haya ni kwa mujibu wa naibu wa rais Kithure Kindiki ambaye alimtangaza mbunge huo kuwa wakala wa Odinga wakati kura hizo zitakapopigwa na marais wa bara Afrika.
Akizungumza siku ya Ijumaa, Kindiki alisema Ichung’wah ataenda Addis Ababa, Ethiopia angalau wiki moja kabla ya uchaguzi, na atarejea tu nchini baada ya Raila kuapishwa, iwapo atashinda.
Naibu rais alifichua kwamba amemtwika Ichung’wah wajibu huo kwa kuwa yeye pia alikesha katika ukumbi wa Bomas kwa wiki nzima kama ajenti wa William Ruto wakati wa uchaguzi wa urais Agosti 2022.
“Nilikuwa ajenti mkuu wa Rais William Ruto kwa siku saba nililala huko (Bomas). Ajenti mkuu wa Raila Odinga mjini Addis Ababa, Ethiopia atakuwa Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah,” Kindiki alisema.
Naibu Rais alizungumza wakati wa mkutano na ujumbe wa viongozi waliochaguliwa, wafanyabiashara na jamii kutoka kaunti ya Kajiado.
Kindiki alibainisha kuwa iwapo Rais William Ruto na Raila wasingekubaliana kufanya kazi pamoja kwa manufaa ya nchi, Kenya isingepata fursa ya kutoa mgombea wa kuongoza Tume ya Umoja wa Afrika.
Alisisitiza kuwa serikali iko tayari kufanya kila iwezalo kuhakikisha Raila anaibuka mshindi katika uchaguzi wa AUC.
“Kama Ruto na Waziri Mkuu Raila wangeendelea na siasa za mgawanyiko za kuwahadaa watu na hakuna kampeni inayoendelea, Kenya ingepoteza fursa tuliyo nayo sasa. Tutatoka nje ya njia yetu. Tunamuombea Raila Odinga. Tunafanya kazi kwa bidii, Ruto anamfanyia kampeni na hatutaacha jambo lolote lile,” akasema.
Raila anakabiliwa na changamoto kutoka kwa wagombea wengine wawili, akiwemo Mohamoud Youssouf wa Djibouti na Richard Randriamandrato wa Madagascar.
Uchaguzi huo utafanyika Februari 25.
Mshindi wa kiti cha mwenyekiti wa AUC anatakiwa kupata uungwaji mkono wa thuluthi mbili ya nchi 55 zinazostahili kupiga kura, ikiwa ni tafsiri ya nchi 33 wanachama wa Umoja wa Afrika.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!