Rigathi Gachagua, naibu wa rais aliyebanduliwa ofisini mwishoni mwa mwaka jana amemshauri aliyekuwa bosi wake William Ruto kutumia nguvu zake kufanyia wananchi kazi badala ya kumjadili.


Akizungumza asubuhi ya Alhamisi moja kwa moja kwenye mitandao wa TikTok, Gachagua alidai kwamba Ruto na wndani wake wa karibu wamemgeuza gumzo kila mahali wanakokwenda na kusahau kuwatumikia wananchi.


Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Gachagua, ambaye katika siku za hivi karibuni amekuwa akifanya misururu ya mikutano ya kisiasa na wanasiasa kutoka Maeneo mbalimbali katika boma lake la Wamunyororo, alimtaka Ruto kukoma kumjadili mara kwa mara na badala yake kujikita katika kuwatumikia wananchi waliomchagua.


 "Rais na timu yake wanaenda katika eneo fulani, na badala ya kuzungumzia barabara, maji, au viwanda vya sukari vinavyopitia nyakati ngumu, wanashughulika kujadili mtu mmoja tu, mimi," Gachagua alisema.


Aliitaka Serikali kuzingatia mambo yanayoonekana kufufua viwanda vya sukari, kuboresha miundombinu ya barabara, upatikanaji wa maji safi na kukabiliana na uhaba wa huduma za afya.


Gachagua pia alibainisha kuwa masuala haya yanafaa kuchukua nafasi ya kwanza kuliko masuala ya kisiasa.


"Tumeona maandishi haya hapo awali. Alipozuru Mlima Kenya, alijua kila barabara kwa jina na kila kijiji kwa moyo. Sasa anafanya vivyo hivyo Magharibi mwa Kenya," Gachagua alisema.


Rais Ruto ambaye yuko eneo pana la Magharibi mwa Kenya kwa ziara ya maendeleo ya wiki moja kuanzia Jumapili iliyopita ametumia siku zake nne kuzindua miradi mbali mbali lakini pia kujinadi kisiasa.


Hizi ni pamoja na kutoa bonasi kwa wakulima wa miwa katika Kampuni ya Sukari ya Mumias, uwekaji lami katika barabara ya Mumias-Musanda, mipango ya kudhibiti mafuriko huko Budalang'i, Mradi wa Umwagiliaji wa Lower Nzoia, na uwekaji jiwe la msingi katika Hospitali ya Khwisero Mother Child Level IV katika Kaunti ya Kakamega.


Hatua nyingine muhimu ni pamoja na kuanzishwa kwa Soko la Kisasa la Luanda katika Kaunti ya Vihiga, kukagua mradi wa Nasewa EPZA huko Busia, na kusimamia mipango ya kilimo.


Hata hivyo, Gachagua aliteta kuwa juhudi hizi zinaweza kugubikwa na misimamo ya kisiasa.


 "Ninawaomba watu wa Magharibi mwa Kenya kuzingatia kuhakikisha maendeleo na wasiyumbishwe vinginevyo," aliongeza.


Naibu rais huyo wa zamani pia alisisitiza kuwa watu wa Magharibi mwa Kenya wanapaswa kuchunguza ahadi zinazotolewa na serikali na kuwawajibisha viongozi.