MAJONZI na simanzi vilitanda katika eneo la Mathare 4A jumatatu asubuhi baada ya baba kuchomwa kisu hadi kufa na vibaka wakati alikuwa akimsindikiza mwanawe kwenda shuleni.
Baba huyo alivamiwa na vibaka majira ya 5:40am wakati alikuwa anamsindikiza mwanawe wa miaka 3 kwenda shuleni.
Wenyeji walisema walisikia kizaazaa na vifijo Jumatatu asubuhi na walipofika eneo la tukio ili kujua chanzo, walijikwaa na mwili wa Michael Oworo ukiwa umetapakaa kwenye dimbwi la damu.
Mwanawe alisimama umbali wa mita chache huku akilia asijue la kufanya baada ya mauaji ya baba yake na kando yake kulikuwa na ‘lunch-box’ yenye ugali na omena kwa ajili ya mtoto huyo shuleni.
Polisi na wenyeji walisema mwathiriwa alikuwa akimpeleka mwanawe katika kituo cha kulea watoto katika eneo hilo wakati mshambuliaji alipomvamia.
Alitaka kumshusha mtoto huyo kituoni kisha aelekee kwenye eneo la ujenzi ambako alifanya kazi ya uashi ili kujikimu kimaisha.
Sababu ya shambulio hilo bado haijajulikana lakini wenyeji walisema mauaji hayo yalitokea katika harakati za wizi.
Mwathiriwa lazima awe amejaribu kupigana na shambulio lililosababisha kifo cha kuchomwa kisu.
Mwili huo ulikuwa na jeraha la kuchomwa kifuani linaloaminika kuchomwa na kitu chenye ncha kali, polisi na mashuhuda walisema.
Kwa mujibu wa majirani hao, marehemu alikuwa single father. Inasemekana alikuwa akiishi peke yake na mtoto huyo tangu alipokuwa na umri wa miezi mitatu.
Wakazi hao walipinga kisa hicho huku wakiibua wasiwasi kutokana na ongezeko la visa vya utovu wa usalama katika eneo la Mathare 4A.
Walisema marehemu alikuwa mfanyakazi wa kawaida kwenye maeneo ya ujenzi na huwa anampeleka mtoto wake katika kituo cha kulelea watoto wadogo ili kumwezesha kujikimu kimaisha.
“Alitaka kumlisha mtoto wake na ndiyo maana alikwenda kwenye maeneo ya ujenzi ili kujikimu. Hili lazima lishughulikiwe,” alisema Felix Popo, mkazi ambaye amekuwa akifanya kazi kusaidia kubadilisha vijana katika eneo hilo.
Wakazi waliokuwa na hasira Jumatatu asubuhi waliwazuia kwa muda polisi kuchukua mwili huo wakipinga ukosefu wa usalama.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!