ALIYEKUWA kiongozi wa kundi haramu la Mungiki, Maina Njenga amejitokeza na kuonekana kupingana vikali na wito wa aliyekuwa naibu raia Rigathi Gachagua kuhusu kuunganisha eneo pana la Mlima Kenya.


Njenga ambaye sasa anaonekana kutetea uongozi wa rais William Ruto anasisitiza kwamba kuondolewa kwa Gachagua serikalini hakumaanishi kwamba eneo zima la Mlima Kenya limeondoka serikalini na kuingia katika mrengo wa upinzani.


Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

“Ningependa kuambia nchi nzima ya Kenya kwamba kuondolewa kwa bwana Rigathi Gachagua sio kuondolewa kwa eneo la Mt Kenya. Eneo la Mlima Kenya litasalia imara na tisti na hatutayumbishwa hata kidogo,” Njenga alisema.


Njenga alisisitiza kwamba si rahisi kwa eneo hilo kujiondoa katika serikali ya rais Ruto kwani karibia asilimia 50 walimpigia kura ya urais.


“47% ya watu wa Mt Kenya walipia hii serikali kura. Na hiyo ndio sababu William Ruto ndiye rais kwa sasa. Na ni vizuri kwetu kuwa ndani ya serikali kuliko kuipiga vita kutoka nje. Kama kuna vita yoyote ambayo tunaenda kupigana basi tutaipigana tukiwa ndani,’ alisema.


Kauli ya Njenga inakuja wakati ambapo inasubiriwa kuona Gachagua akitangaza mweneleo wake mpya wa kisiasa baadae mwezi huu.


Kiongozi huyo alisisitiza kwamba kuondolewa kwa Gachagua serikalini kama naibu rahisi hakuna uhusiano wowote na maslahi ya eneo hilo pana bali ni kwa sababu ya kutokea kutoelewana kibiashara baina yake na viongozi wengine ndani ya serikali ya Ruto.


“Ninajua kwamba kumekuwa na uadui mwingi, kwa sababu ya mwanamume mmoja ambaye aliondolewa serikalini kwa sababu ya sababu zake mwenyewe. Hakuondolewa serikalini kwa sababu ya masilahi ya Mlima Kenya, ni kwa sababu ya biashara ambazo walikuwa wanafanya na viongozi wengine serikalini,” Njenga alisema.