WAVUVI katika ziwa Victoria wameombwa kukomesha tabia ya kunya ziwani humo haswa nyakati za usiku wanapofanya shughuli zao za uvuvi.
Rai hii ilitolewa na afisa wa kaunti ya Homa Bay anayesimamia shughuli za uvuvi, John Agili ambaye alielezea kwamba baadhi ya wavuvi huzama ziwani nyakati za usiku kufanya uvuvi bila mikebe ya kuenda haja, hivyo kuwapelekea kunya ziwani pindi wanapobanwa na haja.
“Tuko na changamoto za uchafuzi wa mazingira, haswa kwa wale wanaoenda kufanya uvuvi na wakati mwingine unapata kwamba wanaenda na kukesha majini usiku kucha na kwa kweli kama hawajijali vizuri, baadhi yao hata hujipata katika majaribu ya kunya majini kama hawana vifaa,” afisa huyo wa kaunti alisema.
Agili alifichua kwamba serikali kwa ushirikiano na washiokadau wengine wamekuwa na mipango ya kuhakikisha usafi wa mazingira yanayopakana na ziwa Victoria ikiwemo kuhakikisha ujenzi wa vyoo kwenye fukwe.
“Nafikiri tumesisitiza kwamba kila kundi ambalo linaenda kufanya uvuvi sharti liwe na njia mwafaka na kujijali ili kwamba wasiweze kuchafua maji. Lakini pia tunafanya kazi na idara yetu ya mazingira kuhakikisha tunafanya usafi mara moja moja kwenye fukwe zetu, pia tumehakikisha kwamba katika fukwe zetu tunajenga vyoo ili kuweza kutumia njia salama za kuweka uchafu wa binadamu ili watu wasinye nje au mahali popote,” alisema.
Afisa huyo alisema kwamba uchafuzi wa mazingira ya ziwani ni changamoto kubwa kwani uchafuzi mwingine ni kutoka nje.
“Ni changamoto kubwa kwa sababu baadhi ya uchafuzi ni kutoka nje, kutoka kwa mito yetu ambayo hutiririsha maji yao kwenda ziwani, watu wanachafua mito na inabeba uchafu huo wote hadi ziwani kwa sababu ya mvua,’ aliongeza.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!