RAIS Ruto amewajibu baadhi ya wanasiasa wanaoeneza uvumi na tetesi kwamba huenda akawa rais wa kwanza kwa Kenya kuongoza kwa muhula mmoja tu.
Akizungumza wikendi iliyopita, kiongozi wa taifa alisema kwamba kauli za kuambiwa hatashinda uchaguzi tena si ngeni kwake kwani hata kabla ya yeye kuwa rais, kuna watu waliokuwa wakifikiria kwamba hangeweza kuwa rais.
Rais Ruto alisema kwamba maneno ya watu na matakwa ya Mungu ni vitu viwili tofauti, akionyesha fahari yake ya kuwa rais wa nchi ya Kenya.
‘Kuna watu wanaongea mambo ya ‘one term, 2 terms, 3 terms’… mimi nataka niwaambie pale nyuma hata hawakufikiria nitakuwa na ‘any term’ lakini Mungu ni nani?” Ruto alihoji.
Kiongozi wa taifa aliradidi maneno yake ya wakati wa kampeni kwamba yeye ni ‘hustler’ akisema kwamba anajivunia kuwa rais wa nchi kwa vile alikuwa ni mtu asiyejulikana.
“Mimi nimefurahi sana kwamba Mungu amenipa nafasi hii niwe kiongozi wa Kenya. Mimi ambaye nilikuwa mtu mdogo asiyejulikana, familia yangu haijulikani, kutoka sehemu ndogo. Mimi ni rais wa Kenya mwenye fahari kubwa,” Rais Ruto alisema.
Mkuu wa nchi alifichua kwamba kuna kazi kubwa sana ambayo Mungu amempa kulifanyia taifa na hatorudi nyuma hadi pale atakapotimiza kusudi la Mungu kwa wananchi wa Kenya.
“Mimi nataka niwaeleze ya kwamba kuna kazi Mungu amenipa nifanye Kenya hii, na nitafanya. Ndio! Mungu amenipa jukumu la kuongoza hili taifa, na wajibu wa kubadilisha Kenya. Na nina kila kusudi la kuhakikisha kwamba tunabadilisha nchi yetu,’ Ruto alisisitiza.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!