KIONGOZI wa chama cha NARC Kenya, Martha Karua amedokeza kuwa na nia ya kuwania urais nchini Kenya, japo hakutangaza ni lini.


Akizungumza katika hafla moja ya mazishi katika kaunti ya Kirinyaga mwishoni mwa juma lililopita, Karua alisema kwamba kwa wakati ufaao, atarejea kwa watu kuwaomba kura za kuwa rais wa Kenya.


Karua alionekana kujutia uamuzi wake wa mwaka 2022, akisema kwamba hatowahi kuwa naibu wa mgombea yeyote wa urais tena.


Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

“Sitakuwa Naibu Wa Mtu Yeyote Tena. Kwa Wakati Ufaao Nitaomba Kura Zenu Kuwa Urais," Martha Karua alifichua.


Kiongozi huyo iwapo atachaguliwa, atakuwa mwanamke wa kwanza kuwa rais wa Kenya, japo hakuweka wazi ikiwa atawania wadhifa huo katika uchaguzi wa 2027.


Itakumbukwa mwaka 2022, Karua aliwania kama naibu kwa kinara wa Azimio, Raila Odinga ambaye alipeperusha bendera ya muungano huo dhidi ya rais wa sasa William Ruto bila mafanikio.


Miaka miwili baadae, Karua alitangaza kujiondoa katika muungano wa Azimio, haswa baada ya kinara wao Raila Odinga kuonekana kushirikiana na rais Ruto kinyume na baadhi ya wanachama wa Azimio.


Lakini Karua hatakuwa mwanamke wa kwanza kuwania urais kwani mwaka 1997, aliyekuwa gavana wa Kitui, Charity Ngilu aliwania urais japo hakushinda na alimaliza wa tatu.


Mpaka sasa, watu kadhaa wametangaza wazi nia yao ya kuwania urais mwaka 2027 wakilenga kumbwaga rais wa sasa William Ruto ambaye anatumai kutetea wadhifa wake kwa miaka 5 zaidi.


Wanaharakati Okiya Omtatah na Morara Kebaso, kila mmoja tayari ameweka wazi nia yake ya kuwania urais huku pia Kalonzo Musyoka na Eugene Wamalwa wakiweka wazi nia zao.


Aliyekuwa naibu wa rais Rigathi Gachagua pia amekuwa akidokeza kuwepo kwa muungano mkubwa utakaofanikisha urais kwao, baada ya kubanduliwa ofisini.