MBUNGE WA KAPSERET Oscar Sudi amedokeza kwamba hata yeye siku za usoni huenda akajaribu karata yake katika kiti cha urais.
Akizungumza na rais William Ruto mwishoni mwa juma wakati wa ziara yake ya maendeleo kwenye bonde la ufa, Sudi alisema kwamba Kenya ni ya kila mtu na kila mtu ana uwezo wa kuwa rais siku moja.
Mbunge huyo alikariri maneno yake kwamba hata watu waruke juu vipi, bado rais Ruto hakuna mahali ataenda, akionyesha Imani kuu kwamba Ruto atachaguliwa tena 2027.
Alitaja uvumi unaoenezwa mitandaoni kwamba rais Ruto anachukiwa na Wakenya kuwa propaganda za watu wa Nairobi tu.
“Si mnajua wale wakora wa mitandao kule Nairobi, wanapiga kelele eti sijui Ruto Must Go sijui nini… mimi niliwaambia waruke juu, waende chini au kando, Ruto hakuna mahali anaenda.”
“Wale wanajifanya wakifikiria kwamba wao tu ndio lazima waongoze hii nchi. Hapana, hata Mluhya au Mturkana anaweza ongoza. Mkenya yeyote ako nja uwezo wa kuongoza. Si hata mimi mtanipatia urais siku nyingine?” Sudi aliuliza umati uliokuwa unamshangilia.
Katika ziara hiyo, rais Ruto pia alimtania mbunge huyo akimtaja kama injinia ambaye hajulikani ni wa nini.
“Ooh, tuko na huyu injinia. Sijui ni injinia wa nini lakini tu ni injinia tusema, anaitwa Oscar Sudi. Nasikia zamani alikuwa area huku sasa amepelea uinjinia mpaka umefika Eldoret. Ahsante sana,” Ruto alisema akimtambulisha Sudi kwa umma kwa njia ya utani.
Kitembo cha Sudi katika Nyanja ya masomo kimekuwa ni mjadala pevu kwa miaka mingi sasa humu nchini.
Mbunge huyo ambaye ni mtetezi mkali wa sera za rais William Ruto alijipata kuwa gumzo la mitandaoni mwaka jana baada ya kufichua kuzawadiwa shahada na chuo kimoja.
Sudi alifichua kwamba alivishwa joho na shahada ya uzamili ya kiheshima na chuo cha Northeastern Christian wakati alipoudhuria hafla ya kufuzu kwa mahafali katika chuo anuwai cha Eldoret.
Shahada hiyo ilivutia joto la kisiasi kutoka kwa baadhi ya watu, hadi ikapelekea mamlaka inayosimamia elimu ya juu CUE kuingilia kati na kutaka shahada hiyo kuchunguzwa na kufutiliwa mbali ikiwezekana
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!