MBUNGE wa Kimilili Didmus Barasa amevunja kimya chake baada ya matokeo ya shule ya upili ya wasichana ya Lugulu kutotoka.


Akizungumza Jumamosi katika hafla moja, mbunge huyo alisema kwamba ana ufahamu kwamba shule ya Lugulu Girls haikupata matokeo yao ya KCSE ambayo yalitangazwa mwishoni mwa juma lililopita na waziri wa elimu, Julius Ogamba Migos.


Mbunge huyo wa UDA alifichua kwamba tayari amefanya mawasiliano na waziri huyo kuhusu hali hiyo ya sintofahamu kwa wanafunzi waliokalia mtihani huo katika shule hiyo na kuelezwa kwamba matokeo yao hayakufutiliwa mbali bali yameshikiliwa tu.


Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Barasa alisema matokeo ya wasichana wa shule ya Lugulu yameshikiliwa tu ili kufanyiwa uthibitisho zaidi lakini si kwamba yamefutiliwa mbali.


Mbunge huyo alidai kwamba matokeo ya wananfunzi hao huenda yameshikiliwa kwa vile walipita sana na kuwashangaza wasahihishaji, lakinj akaahidi yatatolewa hivi karibuni.


“Haya maneno ya Lugulu Girls, ndio mara ya kwanza katika historia ya hii shule, matokeo ya wanafunzi yameshikiliwa. Mimi nimeongea na waziri ambaye anahusika na elimu na amenihakikishia kwamba yale matokeo hayajakataliwa bali yameshikiliwa,” Barasa alisema.


Mbunge huyo alitumia mfano wa VAR katika mpira wa soka kuelezea tofauti kati ya matokeo kushikiliwa na kukataliwa.


“Kuna tofauti kati ya kushikilia matokeo na kukataliwa kwa matokeo. Vile walifanya mtihani, ni kama hawa watoto walipita sana mpaka wale walikuwa wanasahihisha wakasema wawafanyie ‘verification’. Hivyo matokeo yako katika mchakato wa kuthibitishwa,” Barasa alisema.


“Kwa wale ambao mnaelewa kandanda, kama refa hajaona kama bao limeingia au pengine mtu amenawa mpira ndani ya kijisanduku lakini refa hajaona vizuri, anaenda kuangalia kwa kitu kinaitwa VAR. hivyo yale matokeo ya Lugulu Girls wanafunzi walipita sana mpaka wale walimu wakashikwa na wasiwasi mpaka wakasema wanaenda kuangalia kwa kompyuta katika mchakato ambao ni sawa na VAR katika soka,” Barasa alifafanua.


Aliwatoa wasiwasi walimu na wanafunzi hao akisema kwamba KNEC huenda imechelewesha tu kusherehekea kwao kwa matokeo mazuri lakini haijayafutilia mbali kabisa.


“Lakini ninataka kuwapa hakikisho watu wa Bungoma kwamba matokeo ya Lugulu Girls yatacheleweshwa kwa muda mchache tu lakini mwishoni tutakuwa na hayo matokeo. Tumeahirisha kusherehekea kwetu lakini si daima,” Barasa alitoa hakikisho.