SENETA WA KISUMU, profesa Tom Ojienda amedai kwamba kuna uwezekano mkubwa wa chama cha ODM kuungana na chama tawala cha UDA kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.


Akizungumza asubuhi ya Alhamisi katika runinga ya Citizen, Ojienda alisema kwamba ODM kitakuwa mhusika mkubwa wa kuamua njia ambayo matokeo ya 2027 yataelekea.


Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Seneta huyo alisema kwamba katika mazungumzo ya kuunda muungano baina ya ODM na UDA, kuna uwezekano wa kujumuishwa kwa kipengele cha kutaka nafasi ya naibu rais kupewa ODM.


“Tarehe 28 mwezi Februari mwaka huu, Raila Odinga anaenda kuwa afisa mkuu mtendaji wa AUC. Atashinda uchaguzi huo na ataenda Addis Ababa.”


“Njia tunayoeleka 2027 ni kuunga William Ruto kushinda muhula wa pili. ODM atakuwa mchangiaji mkuu na nafikiri makubaliano ya kuunda muungano yatajumuisha uwezekano wa kuwa na naibu rais kutoka ODM. Nafikiri kutoka hapo tutakuwa na nafasi zingine kugawanwa kati ya ODM na UDA kuelekea uchaguzi wa 2027,” profesa Ojienda alisema.


Alipoulizwa kuhusu hatima ya naibu rais wa sasa profesa Kithure Kindiki kwa vile ODM huenda ikatwaa wadhifa anaoushikilia, Ojienda alisema kuwa kuna nyadhifa nyingine nyingi tu na Kindiki hatoshindwa mahali pa kuwekwa.


“Profesa Kindiki najua kwa sasa yuko ndani kabisa ya serikali lakini nafikiri huo ni uamuzi na majadiliano yatakayofanyika wakati huo. Serikali ni kubwa. 2027 ni mchezo mwingine mpya. ODM na UDA vitaelewana na vitaunda muundo ambao utajumuisha nyadhifa za waziri mkuu na mkuu wa mawaziri na hilo litajumuisha kila mtu,” Ojienda alijieleza.