WAZIRI WA ELIMU Julius Ogamba ametangaza kuwa tume ya mitihani ya kitaifa KNEC imeanza mipango ya kuhakikisha wale waliokosa kufanya mitihani ya kitaifa ya KCSE au wale wanaotaka kurudia inafanyika.


Kwa mujibu wa waziri Ogamba, KNEC itahakikisha wale wanaotaka kurudia KCSE na wale waliokosa kufanya mitihani hiyo kutokana na sababu mbalimbali wanaikalia mitiani hiyo mwezi Julai.


Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Ogamba alisema ii itakuwa inafanyika kila mwaka mwezi Julai ili kuhakikisha kila mtu anapata haki ya kukalia mtihani huo wa kumaliza shule ya upili.


“Ningependa kusema kwamba serikali inaendelea kuboresha njia ya kuhakikisha viwango vya juu katika mazingira ya kufanyika kwa mitihani ya kitaifa.”


“Kuanzia mwaka huu na kufuatia majadiliano ya kina na washikadau wote katika elimu, ningependa kutangaza kwamba KNEC itatoa mwongozo wa mitihani ya KCSE kufanyika Julai kila mwaka,’ Ogamba alisema.


“Mitihani hiyo itawalenga wale watahiniwa wanaotaka kurudia KCSE na wale waliokosa kukalia mitihani hiyo kutokana na ugonjwa, au ugumu mwingine usiotarajiwa. Watu wazima pia wanaotaka kufanya mitihani hiyo wanaweza jiandikisha kwa mitihani hiyo ya awamu ya Julai kuanzia mwaka huu,” Ogamba aliongeza.


Waziri huyo alitoa tangazo hili Alhamisi mchana wakati wa kutangazwa rasmi kwa matokeo ya KCSE ya mwaka 2024.


Jumla ya watahiniwa 962,512 walikalia mitihani hiyo ambayo imekuwa ikifanyika kwa miaka 35 sasa na ambayo itaacha kufanywa mwaka wa 2027 na kuachia nafasi kwa mtaala mpya wa CBC kwa ukamilifu.