ERIC WAMUMBI, Mbunge wa Mathira, ambako ni Eneobunge la aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua ameibua madai mapya dhidi ya kiongozi huyo akimhusisha na msururu wa utekaji nyara wa vijana kadhaa humu nchini.
Katika barua aliyoiandikia idara ya DCI, Wamumbi alimtuhumu mtangulizi huyo wake katika Eneobunge la Mathira kwa kuhusika katika kuwateka nyara vijana na kisha kuwaficha katika mgahawa wa kifamilia wa Olive Gardens jijini Nairobi.
Wamumbi aliitaka DCI kuanzisha uchunguzi dhidi ya shughuli zinazofanyika katika mgahawa huo, akidai kuwa huenda vijana wanaoripotiwa kupoteza wanafichwa katika hoteli hiyo.
“Ninaandika kuomba uchunguzi dhidi ya shughuli zinazofanyika katika mgahawa wa Olive Gardens Nairobi, kuhusiana na utekaji nyara unaoendelea. Uku tukiendelea kuhuzunika na wazazi ambao wako na wasiwasi kuhusu waliko wanao, ninaamini baadhi ya watu wanafanya mikutano katika hoteli hiyo wakipanga utekaji nyara feki ambao unanuia kuchochea umma,” Barua ya Wamumbi ilisoma.
Aliendelea kwa kumtag Gachagua na kumtaka kuachilia vijana ambao alimtuhumu kuwateka nyara, akisema kwamba yeye ni baadhi ya watu wanaomjua vizuri sana naibu rais huyo wa zamani.
“H.E. Rigathi Gachagua, EGH, Waachilie watoto wote ambao umekuwa ukiwashikilia kwenye hoteli ya Olive Gardens na ukomeshe mchezo wa kuigiza. Wale wa kijijini kwako tunakujua na maigizo. Wacha kutesa wazazi sababu ya siasa bwana,” Wamumbi aliongeza.
Barua yake kwa DCI inajiri siku chache tu baada ya baadhi ya viongozi akiwemo mbunge wa Kikuyu ambaye pia ni kiongozi wa wengi katika bunge, Kimani Ichung’wah na katibu wa muungano wa wafanyikazi COTU, Francis Atwoli kudai kwamba baadhi ya vijana wanajificha wakidai kutekwa nyara.
Wiki iliyopita, Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse pia alitoa taarifa sawia na hiyo akidai kwamba utekaji nyara unaoendelea unafanywa na Rigathi Gachagua.
Hata hivyo, ni madai ambayo Gachagua ameyapinga vikali akisema kwamba serikali ina wajibu wa kulinda kila Mkenya na kukomesha visa vya vijana kutoweka.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!