GAVANA wa Murang’a Irungu Kang’ata ametangaza mpango
wa serikali yake kuqanza kuwalipia karo yote wanafunzi werevu katika shule za
upili za kutwa kuanzia Januari.
Hatua hiyo inalenga kuwapa motisha wanafunzi katika shule za sekondari za kutwa, ambapo wengi wa wanafunzi walioandikishwa katika shule hizo wanatoka katika mazingira duni.
Akizungumza aliposambaza chakula kwa mamia ya wakazi katika uwanja wa Ihura kuadhimisha msimu wa sherehe, gavana huyo aliona baadhi ya wanafunzi katika shule za kutwa wanachangamka, lakini walikosa usaidizi wa kujiunga na shule za kitaifa na zile za ziada.
“Tunataka kuhakikisha wanafunzi wanaofanya vyema katika shule zetu za kutwa wanapata motisha na pia kuendeleza masomo yao bila changamoto.”
"Kuanzia Januari mwaka ujao, wanafunzi waliochaguliwa watasoma bila malipo kwani karo zao zitalipwa na serikali ya kaunti," Kang’ata asema.
Mkuu huyo wa kaunti aliongeza kuwa mpango huu utawapa changamoto wanafunzi kuchukua elimu kwa uzito na kuwa washindani katika ngazi ya kitaifa pia.
Kang’ata alitaja baadhi ya shule za kutwa za eneo hilo ambazo zimekuwa zikitoa sehemu ya kumi ya wanafunzi kujiunga na vyuo vikuu.
“Tuna shule za upili za Karega na Mukangu kati ya zingine ambazo katika miaka ya nyuma zimekuwa zikitoa wanafunzi wenye alama zinazohitajika kujiunga na vyuo vikuu. Hili limetusukuma kuwafikiria wanafunzi katika shule wanaohitaji kuhamasishwa ili kushindana na wale wa shule za kitaifa na za ziada,” aliongeza.
Kwenye programu zingine za ufadhili wa masomo zilizoanzishwa na serikali ya kaunti, Kang’ata alihakikishia zitaendelea kutolewa ili kuhakikisha wanafunzi kutoka familia maskini hawapotezi nafasi za kuendelea na masomo yao.
Wakati uo huo, Kang’ata alisisitiza hatua ambazo utawala wake umechukua ili kuboresha huduma za afya katika kaunti hiyo.
Alibainisha kuwa serikali ya kaunti inapanga kuajiri wauguzi zaidi na kujenga vituo zaidi vya afya katika wadi tofauti ili kuimarisha utoaji wa huduma za afya katika kaunti hiyo.
“Ifikapo Januari, tutakuwa tumepunguza msongamano katika vituo vyetu vya afya. Kwa mfano, mipango inaendelea ya kufungua zahanati ya Mukuyu na kuajiri wauguzi wapya katika zahanati nyingine mpya katika wadi mbalimbali,” akasema.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!