WAZIRI wa madini na uchumi wa baharini Ali Hassan Joho amesisitiza kwamba kauli zake ni sawa na tamko la serikali pindi anapozungumza popote.


Akizungumza katika kaunti ya Tana River katika shughuli ya Danson Mungatana, waziri Joho alifafanua kauli ya naibu rais Kithure Kindiki kuhusu jinsi serikali imerahisisha maisha ya mwananchi wa kawaida katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.


Joho akiunga mkono kauli za naibu wa rais, alisisitiza kwamba maadamu yeye sasa ni waziri, anapozungumza ni sawa na serikali imezungumza.


Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

“Mheshimiwa naibu wa rais amesema hapa kwamba anataka yeye na rais wetu William Ruto kuhakikisha kwamba wanaweka pesa mifukoni mwa watu. Mnajua mimi ni waziri sasa hivi. Ama hamuelewi hilo? Mimi nikiongea hapa, mimi ni serikali kamili. Lazima tuweke mipango ya kuwaelewesha,” Joho alisema.


Joho alichukua fursa hiyo kuelezea majukumu yake katika wizara ambayo alirithi kutoka kwa Salim Mvurya ambaye hivi majuzi amehamishiwa tena katika wizara ya michezo na Sanaa.


“Mimi binafsi katika wizara yangu ambayo nimerithi kutoka kwa ndugu yangu Salim Mvurya, kuna mambo ya uvuvi, madini, na uchumi wa baharini. Hapa mimi nataka tukubaliane kwamba tumesikilizana na mheshimiwa Ali Wario barabara itakuja hapa ili wavuvi wetu wakivua samaki wanapata soko,” Joho alijipigia debe.


Kauli ya gavana huyo wa zamani wa Mombasa inajiri wiki chache baada ya kuvutia maoni kinzani mitandaoni kutokana na kauli zake za kuwashambulia kwa maneno wanaharakati wa mitandaoni wanaokosoa serikali.