MUHOOZI Kainerugaba, mwanawe rais wa muda mrefu wa Uganda Yoweri Museveni amempigia debe mama yake Janet Museveni kumrithi baba yake na kuwa rais wa kwanza wa kike Uganda.


Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Kupitia ukurasa wake wa X, Kainerugaba ambaye pia ndiye mkuu wa majeshi ya Uganda alisema kwamba hajawahi ona mwanamke mrembo duniani kama mama yake na kusema kwamba anastahiki kuwa rais ajaye wa taifa hilo.


Uganda wanatarajiwa kuelekea katika uchaguzi mkuu 2026 ambapo inaarifiwa Museveni huenda hatawania baada ya kuwa rais kwa miaka 38, na mwanawe anataka mamake kuchukua usukani.


“Mbali na Charlotte, sijui mwanamke katika sayari hii ambaye ni mzuri zaidi kuliko mama yangu! Binafsi namuunga mkono kuwa Rais wa kwanza mwanamke wa Uganda,” Muhoozi Kainerugaba alisema kupitia ukurasa wake wa jukwaa la X.



Kwa muda mrefu, Muhoozi amekuwa akitajwa kuwa mrithi wa rais Museveni pindi mzee huyo atakapostaafu kutoka siasa baada ya kuingia ikuluni mwaka 1986.


Hata hivyo, hivi majuzi, Kainerugaba alisema kwamba hana haja ya kuwania dhidi ya baba yake na kuonyesha kutosheka na wadhifa wake wa mkuu wa majeshi.


Mnamo Septemba, Muhoozi alisema anaangazia jukumu lake katika jeshi na kumuidhinisha Museveni katika uchaguzi ujao.


 


“Ningependa kutangaza kwamba sitakuwa kwenye karatasi ya kura mwaka wa 2026. Mwenyezi Mungu aliniambia nizingatie Jeshi Lake kwanza. Kwa hivyo, ninaidhinisha kikamilifu Rais Yoweri Museveni katika uchaguzi ujao,” Muhoozi alisema.


Hata hivyo, alisema nchi hiyo haitatawaliwa na kiongozi wa kiraia baada ya babake.


Muhoozi alisisitiza kuwa vikosi hivyo havitaruhusu raia kuchukua madaraka baada ya Museveni, akiongeza kuwa rais ajaye lazima atoke katika vyombo vya usalama vya Uganda.


“Hakuna raia atakayeongoza Uganda baada ya Rais Museveni. Vyombo vya usalama havitaruhusu. Kiongozi atakayefuata atakuwa askari au polisi,” alisema.


Museveni ndiye rais wa 4 barani Afrika kati ya marais waliohudumu kwa muda mrefu zaidi madarakani.


Mnamo Januari 1986, baada ya vita kali ya Kampala, Museveni aliapishwa kama rais. Akiwa rais, Museveni alikandamiza uasi wa Uganda na akasimamia kuhusika katika Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Rwanda na Vita vya Kwanza vya Kongo. Aliamuru kuingilia kati dhidi ya Lord's Resistance Army katika juhudi za kukomesha uasi wao.