MWANAUME mmoja raia wa Nigeria ambaye amekaa kwa muda wa miaka 10 kwenye hukumu ya kifo kwa kuiba kuku na mayai ameahidiwa kusamehewa na gavana wa jimbo la Osun kusini-magharibi.


Segun Olowookere alikuwa na umri wa miaka 17 mwaka wa 2010 alipokamatwa pamoja na mwandani wake, Morakinyo Sunday.


Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Inasemekana walishambulia nyumba ya afisa wa polisi na mtu mwingine wakiwa na bunduki ya kizamani ya mbao na upanga lakini wakatoroka tu na kuku.


Mnamo 2014, Jaji Jide Falola wa Mahakama Kuu ya Jimbo la Osun aliwahukumu wawili hao kifo kwa kunyongwa baada ya kuwapata na hatia ya kuvunja kwa nguvu nyumba ya afisa huyo wa polisi na kuiba mali yake.


Kulikuwa na kilio kote Nigeria wakati huo kwani wengi walihisi hukumu hiyo ilikuwa kali sana.


Wawili hao baadaye walihamishwa hadi katika gereza maarufu la ulinzi mkali la Kirikiri katika jimbo la Lagos ambako wamekuwa katika mrengo wa kunyongwa.


Katika taarifa Jumanne, gavana Ademola Adeleke aliagiza Olowookere asamehewe kwani ni muhimu kulinda utakatifu wa maisha.


“Nimemuagiza Kamishna wa Haki aanzishe michakato ya kutoa haki ya huruma kwa kijana huyo.”


"Osun ni nchi ya haki na usawa. Lazima tuhakikishe usawa na ulinzi wa utakatifu wa maisha," gavana alichapisha kwenye X.


Hatima ya Morakinyo Sunday, ambaye alihukumiwa kifungo pamoja na Olowookere, haijulikani kwa vile jina lake halikutajwa kwenye taarifa hiyo.


Kwa miaka mingi, wazazi wa Olowookere, mashirika ya kutetea haki za binadamu na Wanigeria wengine wamepigania kuachiliwa kwake.


Wazazi wake hivi majuzi walikuwa kwenye podikasti ambapo walilia na kuomba mtoto wao wa pekee asamehewe.


Anatarajiwa kuachiliwa mapema mwaka wa 2025.


Nigeria haijatekeleza hukumu ya kifo tangu mwaka 2012 lakini kwa sasa kuna zaidi ya watu 3,400 wanaosubiri kunyongwa.