NAIBU wa rais Profesa Kithure Kindiki amepuuzilia
mbali uvumi kwamba alihusika katika mchakato wa kubanduliwa ofisini kwa
mtangulizi wake, Rigathi Gachagua.
Akizungumza na waandishi wa Habari jioni ya Alhamisi katika makao rasmi ya naiobu wa rais ya Karen, kuangazia mafanikio yake ndani ya siku 50 kama DP, Kindiki alisema kwamba Gachagua anasalia kuwa rafiki yake mkubwa.
Kindiki alisema kwamba si vizuri kwa watu kujaribu kumfananisha na Gachagua, akisema kwamba yeye anamheshimu Gachagua na atasalia kuwa rafiki yake muda wote.
“Itakuwa vibaya kwangu kujilinganisha na mtu yeyote ambaye hapo awali alichukua afisi hii au na aliyekuwa naibu wa rais. Sina sababu ya kumuudhi mtu yeyote,” alisema.
“Uongozi unaainishwa na maadili na vigezo fulani na uniruhusu nisimjadili kaka yangu Rigathi Gachagua kwa sababu ni rafiki yangu na hujawahi kunisikia nikimsema vibaya popote pale alipokuwa ofisini au hata baada ya kuondoka madarakani, ni makosa."
DP Kindiki alijitenga na masaibu yaliyomkumba Gachagua kupelekea kubanduliwa kwake ofisini mapema mwezi Oktoba.
Kulingana na aliyekuwa waziri wa Mambo ya Ndani, Mahakama ya Juu ilijitangaza yenyewe katika kesi hiyo, na hivyo kufunguliwa mashtaka ilikuwa suala la hukumu ya mahakama.
Akitoa mfano wa kesi ya Gavana wa Meru Kawira Mwangaza ambaye amenusurika katika kesi mbili za kuondolewa madarakani, Kindiki alidai kuwa hukumu hazipaswi kulinganishwa kwa sababu ziko chini ya "maamuzi ya kipekee ya mahakama."
"Kesi hizo mbili zilinufaika na vizuizi vya mahakama. Tofauti pekee ni katika moja, baada ya kusikilizwa kwa suala kati ya vyama kuhusu kama agizo hilo lihifadhiwe au la,” alisema.
“Katika kesi moja, mahakama ilipata zuio hilo lilihitaji kuondolewa huku katika kesi nyingine mahakama ikaona kwamba hakukuwa na haja ya kuondoa zuio hilo na hutokea mahakamani wakati wote si tu nchini Kenya bali duniani kote. Kwa hakika, matokeo ya mahakama mara nyingi yanabatilishwa na mahakama inayofuata siku yoyote ile, na hivyo hakuna kutofautiana; hayo ni mazoea ya mahakama.”
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!