ALIYEKUWA naibu wa rais, Rigathi Gachagua amnemtaka
rais Ruto kuwa makini na lugha ambayo anatumia kuwazungumzia wanancvhi.
Akizungumza Jumapili katika ibada ya kanisa la Kinunga Baptist huko Mukurweini, kiongozi huyo wa zamani alisema kuwa rais hahitaji kuonyesha au kutumia lugha ya hasira anapozungumzia kuhusu masuala yanayowakumba wananchi.
“Hakuna haja ya kutukana raia. Hawa wananchi wakitoa maoni yao, wewe sikiliza tu hata kama hupendi hakuna haja ya kusema wako na mapepo kwa sababu hakuna haja,” Gachagua alisema.
“Kama ni haya mambo ya chanjo kwa ng’ombe unasema hawa watu ni wajinga, hakuna haja ya kutukana watu,” aliongeza ushauri.
Gachagua alisema kuwa kiongozi wa nchi anaonyesha picha isiyofaa kuwaingilia kimaneno hadi wahubiri wa makanisa, akimsuta pia kwa kile alisema ni kuwageuka watu wa Mlima Kenya ambao wengi walimpigia kura nyingi baada ya kushawishika na ajenda zake.
“Hata juzi niliona wahubiri wakitukanwa, eti wengine hawajasoma. Sasa baadhi yetu hatuna uwezo wa kujua mhubiri amesoma na yule hajasoma, hakuna haja ya kutumia lugha chafu. Wewe waheshimu tu wananchi wa Kenya kwa sababu hicho ndicho kitu sahihi tu cha kufanya,” Gachagua alisisitiza.
Kauli ya Gachagua inajiri siku chache baada ya rais Ruto kudai kwamba kuna pepo mbaya ambayo imeingia Wakenya ambayo ni ya kupinga kila mradi wa serikali.
Ruto alisema kuwa hata wale wanaofurahi kusitishwa kwa mkataba wa kampuni ya Adani kupanua uwanja wa ndege wa JKIA, wengi wao hawajawahi fika katika uwanja huo.
“Mimi nataka niwaulize Wakenya, tafadhalini, kuna pepo chafu ya upingsmizi, kupinga kila kitu. Kiwanda kama hiki, watu wanapinga, ujenzi wa nyumba za bei nafuu wanapinga, chanjo ya ng’ombe kuondoa magonjwa, wanaipinga, kubadilisha mfumo ndio tuweze kuokoa vyuo vyetu ambavyo vilikuwa vinakwama wanapinga…”
“Wanapinga hata miradi yoyote ya serikali. Mambo ya bima ya afya kwa wote wanaipinga, mambo ya afya wanapinga. Sasa mimi nauliza, hii pepo chafu nafikiri hata imefikia hatua wanapinga hata matoleo kanisani,” Ruto alisema huku hadhira ikicheka.
Ruto alisema kuwa pepo hiyo ya kupinga kila kitu inahitaji maombi kwa taifa, akiwarai wananchi kuombea nchi.
“Hii pepo ya kupinga kila kitu, tuombee nchi yetu. Ama niaje jamani? Hivyo wale wanapinga kila kitu sijui mitandaoni, sijui wapi tunawaambia shetani ashindwe,” Ruto alikariri.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!