Mwanzilishi mwenza wa Bonfire Adventures Simon Kabu amepuuzilia mbali madai ya kuvujisha video za CCTV zilizoonyesha ambaye alionekana kama mke wake wa miaka mingi Sarah Mtalii akimshambulia mwanamke mwingine ndani ya nyumba yao.
Akizungumza katika mahojiano na Eve Mungai mnamo Alhamisi jioni, tajiri huyo alieleza kuwa video hizo zilitolewa wakati wa uchunguzi baada ya anayedaiwa kushambuliwa kuripoti kisa hicho kwa polisi.
Simon alionekana pia kusisitiza kuwa mwanamke aliyeonekana kushambuliwa kwenye video hiyo alikuwa ni yaya wake.
“Jambo hilo lilipotokea, yule yaya alienda katika kituo cha polisi na kuandikisha ripoti. Ilikuwa ni jambo linalochunguzwa,” Simon Kabu alisema.
Mfanyibiashara huyo na mzazi mwenzake Sarah Kabu ambaye kwa sasa anajitambulisha kwa jina la Sarah Mtalii wanaaminika kuwa katika mchakato wa talaka baada ya ndoa yao ya zaidi ya miaka 15 kugonga ukuta.
Mjasiliamali huyo hata hivyo alionekana kukwepa kuzungumzia maswala kati yake na mzazi mwenzake akitaja heshima kwake kwani ndiye mama wa watoto wake.
"Sitaki kujadili hilo kwa sababu kuna mambo mengi yanafanyika na ukweli hatimaye utasemwa," alisema.
Haya yanajiri takriban wiki moja baada ya video kuibuka ikimuonyesha Sarah akihusika katika ugomvi mkali na msichana mmoja katika nyumba yake ya zamani.
Katika video hiyo, aliyeonekana kuwa Sarah alionekana akimsukuma mwanamke huyo nje ya nyumba, kabla ya Simon kuingilia kati. Licha ya jitihada za kuzuiwa, Sarah alionekana kukataa, akijaribu mara kwa mara kumkabili mwanamke huyo.
Video hiyo ilizua uvumi mwingi mtandaoni, huku wengine wakidai kuwa mwanamke huyo alikuwa msaidizi wa nyumbani wa Sarah.
Akijibu, Sarah aliweka wazi uamuzi wake wa kuondoka katika nyumba yake ya awali na kuweka rekodi sawa kuhusu uvumi uliokuwa ukiendelea.
"Kuna msichana anasema ni housegirl wangu nilimchapa kule tulitoka... kunaitwa kwa Pharaoh ama Misri. Ati nilikuwa Misri nikimchapa," Sarah alisema kwenye video hiyo, akilinganisha nyumba yake ya awali na Misri.
Kisha akawatambulisha wasaidizi wake wawili wa nyumbani waliomtumikia kwa muda mrefu, Caroline Atieno na Lillian Aoko, ambao wamekuwa naye kwa miaka minane na kumi, mtawalia.
Sarah kisha akaendelea kumtaka mwanamke huyo ambaye hakujulikana ajitokeze na kujidhihirisha:
"Nataka atoke aeleze yeye ni nani ndani ya nyumba hiyo au alifikaje kwenye hiyo nyumba. Au Simon aeleze ni nani huyo bibi ndani ya nyumba hiyo," alisema.
Pia aliibua madai kwamba Ilikuwa ni mtu mmoja tu aliyeweza kufikia mfumo wa CCTV uliowekwa ndani ya nyumba yao.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!