SIKU mbili baada ya
kufichua kuwepo kwa mkutano baina yake na rais mstaafu Uhuru Kenyatta, rais
Ruto amefichua sababu zilizomsukuma kumtafuta nyumbani kwake Ichaweri.
Akizungumza na Jumanne, Ruto alisema kwamba hatua yake ya kumtafuta rais mstaafu ni kulenga kuzika tofauti zao katika kaburi la sahau na kuganga yajayo, lengo kuu likiwa ni kuleta umoja wa taifa kwa kuwahusisha viongozi wote.
Kiongizi wa taifa alikiri kwamba ni kweli alimtafuta rais mstaafu ili kutafuta mwafaka kuhusu mustakabali wa nchi.
“Ndio sababu kwamba ninafanya kazi na waziri mkuu wa zamani, ndio sababu nilimtafuta rais mstaafu, na ndio sababu nitawatafuta viongozi wote wa kila aina ili kwamba tuweze kujenga nchi ambayo sisi wote tuna Imani nayo,” alisema Ruto.
“Ni lazima tuendelee kujenga madaraja ya kutuunganisha kuliko kujenga kuta za kutugawanya. Ni lazima muda wote tujenge nguvu ya pamoja tunaposonga mbele,” Ruto aliongeza.
Hata hivyo, katibu mkuu wa chama cha Jubilee Jeremiah Kioni alisisitiza kwamba mkutano wa Ruto na Uhuru haukuwa na lengo la kukijumuisha chama cha Jubilee ndani ya Serikali.
“Hatufanyi mazungumzo na wewe ili sisi tuingie serikalini, tunafanya mazungumzo kwa sababu ni muhimu kwa sisi wote kama Wakenya kuzungumza na kila mmoja.”
Hata hivyo, mshauri wa rais katika masuala ya kiuchumi, Moses Kuria ameonekana kukinzana na Kioni, akisema kwamba ni muda wa kukifufua chama cha Jubilee huku akitoa maoni kwamba ni muda wa kurejesha mswada wa BBI.
“Namrai rais William Ruto na rais mstaafu Uhuru Kenyatta kujadiliana kuhusu uongozi wa nchi na kufufua BBI, kuipa nchi katiba ambayo itazingatia masuala ibuka ya taifa na jamii. Awamu ya pili ya BBI inahitajika kwa haraka na haiwezi subiri,” Kuria alisema.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!